Thursday 20 June 2013

Waliovamia mgodi Handeni waomba muda zaidi




Waliovamia mgodi Handeni 

waomba muda zaidi

kuondoka



Wachimbaji wadogowadogo wa madini aina ya dhahabu, waliopo katika machimbo maarufu ya Magambazi Magamba wilayani Handeni, wameiomba Serikali kuwapa muda wa miezi sita, kabla ya kuondoka katika eneo hilo.
Wameamua kufanya hivyo kutokana na kutakiwa kuondoka kwenye machimbo hayo kwa hiari ifikapo Machi 21, mwaka huu na kuonywa kwamba kama wasipotekeleza agizo hilo wataondoshwa kwa nguvu, kwa madai kwamba eneo hilo linamilikiwa na mwekezaji.
Ombi hilo walilitoa juzi kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea machimbo hayo na kujionea mitambo ya wachimbaji hao ikiendelea kusaga mawe ya madini hayo, huku wengine wakijiandaa kuondoka.
“Sisi tumekaa hapa kwa miaka karibu 10 kwanza hata sisi tumepachoka kuishi hapa, tunafahamu kwamba hapa tulipo ni kwa mtu ambaye ana miliki eneo hili.
Lakini kwa vile tuna mitambo yetu na rundo la mawe kama mnavyoona, hatuwezi kuondoka kwa muda wa siku hizi nne tulizopewa ambazo zimeisha,” alisema Andrew Rulu.
Katibu wa wachimbaji hao katika machimbo hayo John Denis, alisema kwamba hawakatai kuondoka hapo, ila wapewe muda kwa ajili ya kuhamisha virago vyao, ili kwenda kuanza maisha ya kuwekeza sehemu nyingine.
Akizungumzia wachimbaji hao, mmiliki wa eneo hilo Rais wa Kampuni ya Canaco nchini, Denis Dillip, alilalamikia baadhi ya viongozi wa juu serikalini, kwa kushindwa kuwaondoa wachimbaji hao tangu mwaka 2008, akisema kuwa ana shaka kwamba ndani yake kuna mkono wa rushwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Muhingo Rweyemamu, alisema kwamba hataongeza muda mwingine wa wachimbaji hao kuondoka, akisema kwamba tayari walishapewa barua za kutakiwa kuondoka tangu mwaka 2009/10, lakini hawakutii.
Rweyemamu alisema wachimbaji wenye Leseni wamewapangia maeneo mengine ya kuchimba, kwa madai kwamba hawawezi kutoa leseni juu ya leseni.    

No comments:

Post a Comment