Monday 3 June 2013

KINANA ANENA



 KINANA AASA WAGOMBEA UONGOZI CCM
Songea. Katibu Mkuu wa CCM, Abdul rahman Kinana amewaonya watendaji wa chama hicho nchini wajiepushe kuwa mawakala wa kutengeneza safu za kugombea uongozi ndani ya chama ikiwamo ya urais 2015.
Alionya kuwa iwapo watu hao watagundulika watachukuliwa hatua na kuwataka waache mara moja.
Kauli hiyo ya Kinana imekuja siku chache baada ya hivi karibuni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kunukuliwa na gazeti hili akieleza kuwa wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kinana alisema hayo jana wakati akifungua mkutano wa ndani wa chama, Wilaya ya Songea Mjini uliolenga kutathimini utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ambao ulihudhuriwa na mamia ya viongozi wa CCM wakiwamo mabalozi, viongozi wa mashina na matawi.
“CCM itaendelea kuwa na imani kubwa kwa wananchi ambao katika uchaguzi wa mwaka 2010 walikipa ushindi wa kishindo kwa wagombea wa udiwani, ubunge na urais hivyo ni lazima kuwakemea baadhi ya watu wanaojifanya kuwa ndiyo mabingwa wa kutengeneza safu ya ugombea wa udiwani, ubunge na urais mwaka 2015,” alisema Kinana.
Amewataka wanachama wa CCM kuwa kifua mbele kwa kujivunia miradi mbalimbali ikiwamo ya barabara zinazojengwa na shule za kata ambazo zimeonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha elimu kwa kila Mtanzania na kwamba tatizo la uhaba la walimu wa masomo ya Sayansi ifikapo 2015 litakwisha na litabaki kuwa ni historia kwani CCM inaendelea kusimamia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2010.
“Msiwasikilize wanaobeza kuwa eti shule za kata hazifai na ninyi wanaCCM muwaulize shule zao zinazofaa walizojenga ziko wapi halafu endeleeni kuwadharau kwa kuwa vyama vyao vya siasa havina mwelekeo wowote na havina msaada kwa jamii na badala yake vimekuwa ni kubeza kazi zinazofanywa na Serikali ya CCM,” alisema Kinana.    

No comments:

Post a Comment