Saturday 27 July 2013

Walioiba fedha ujio wa marais wabanwe



Walioiba fedha ujio wa

 marais wabanwe

 



Kama kuna jambo ambalo linamshangaza kila mgeni anayetembelea nchi yetu, jambo hilo ni umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi, huku nchi ikiwa na utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali za kila aina pengine kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika.
Wananchi wengi pia wamekuwa wakitatizwa na hali hiyo, hivyo kuuliza maswali mengi pasipo kupata majibu. Lakini jambo moja ambalo wananchi wengi wamelibaini kama moja ya sababu kubwa za kuwapo umaskini wa kutisha nchini ni kuporomoka kwa maadili ya viongozi na kupotea kwa uzalendo.
Ni vitendo hivyo ambavyo vimetuletea laana na kudidimiza uchumi wa nchi. Baya zaidi ni pale wengi wa wale waliopewa dhamana ya kuongoza nchi na kulinda rasilimali zake, ndiyo walewale wanaowageuka wananchi na kuhujumu uchumi kwa vitendo vya wizi na ubadhirifu wa rasilimali hizo. Wananchi wameachwa njiapanda wakiwa katika umaskini wa kutisha na kulazimika kuishi kama wakimbizi katika nchi yao.
Tumelazimika kusema hayo kutokana na vitendo hivyo kuendelea kushamiri kiasi kwamba wananchi hawaoni tena kama viongozi wana uchungu na nchi. Kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kwamba Sh8 bilioni zilizotumika wakati wa Mkutano wa Smart Partnership uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni zilifujwa na baadhi ya watumishi wa Serikali, ni kauli inayodhihirisha kwamba nchi yetu sasa ni mateka wa kudumu wa ufisadi na haina tena matumaini ya kujenga uchumi shirikishi unaotumia rasilimali za nchi kuwanufaisha wananchi.
Tunampongeza Waziri Sitta kwa kumfunga paka kengele na kukataa kuficha maovu kwa kisingizio cha uwajibikaji wa pamoja. Bila shaka kauli yake hiyo itakuwa imewaudhi na kuwafadhaisha wenzake wengi katika Baraza la Mawaziri ambao wamekuwa wakiona ufisadi ukifanyika lakini wanafunika kombe ili mwanaharamu apite. Dhana ya uwajibikaji wa pamoja imekuwa ikipotoshwa makusudi. Viongozi wengi wametumia dhana hiyo kuficha maovu, hata pale maovu hayo yanapokuwa na viashiria vya kuiangamiza nchi na watu wake.
Tunakubaliana na Waziri Sitta kwamba ufisadi huo lazima uchunguzwe na hatua madhubuti na stahiki zichukuliwe. Tunakubaliana naye pia kwamba CAG ndiye achunguze kashfa hiyo kwa sababu amejijengea sifa ya uadilifu, hivyo ripoti yake haitegemewi kumlinda mtu yeyote, wala kuficha jambo lolote chini ya zulia.
Umuhimu wa kauli ya Waziri Sitta ni kwamba imezionyesha mamlaka husika mahali pa kuanzia. Kwamba fedha hizo zilifujwa na baadhi ya watumishi wa Serikali ambao walijitengenezea kampuni bandia za mapambo, machapisho na nyingine ambazo hazijasajiliwa. Katika hali hiyo, hakuna anayeweza kubisha kwamba watumishi hao walifanya ufisadi huo kwa baraka na ushirikiano wa vigogo wa ngazi za juu kabisa katika Serikali.
Serikali ina hali mbaya sana kifedha hivi sasa, lakini ndio kwanza mafisadi wanazidisha kasi ya kuihujumu. Zipo pia habari zisizoacha shaka kwamba mabilioni ya fedha pia yalifujwa na mafisadi serikalini wakati wa mkutano wa Wake za Marais barani Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam na wakati wa ziara za marais Baraka Obama wa Marekani na Rais Xi Jinping wa China hapa nchini. Kashfa hiyo inajulikana vizuri serikalini, lakini mamlaka husika zimekaa kimya pengine kwa kisingizio cha uwajibikaji wa pamoja.

No comments:

Post a Comment