Thursday 18 July 2013

UHAMIAJI MKOA KAGERA


KUZINDUA KAMPENI

NEMBO YA UHAMIAJI
            Idara ya Uhamiaji mkoani Kagera inatarajia kuzindua kampeni kabambe dhidi ya wahamiaji haramu mkoani hapa kuanzia Jumatatu wiki ijayo mjini Bukoba. Akiongea na bloga wetu, Afisa Uhamiaji mkoa wa Kagera DCIS. George Kombe alisema kwamba kwamba kampeni hiyo itazinduliwa ikiwa na lengo la kuwaelimisha wananchi wa mkoa huu madhara ya wahamiaji haramu.

"Tunaanza kampeni dhidi ya wahamiaji haramu kwa kuwaelimisha wananchi madhara ya wahamiaji haramu nchini kwetu hususan mkoa wetu wa Kagera ambao umeathirika sana na tatizo la kuwa na wahamiaji haramu wengi kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Uganda. Pamoja na elimu itakayotolewa, pia tumeandaa mabango na vipeperushi ambayo tutasambaza kila pembe ya mkoa huu ili kuwafanya wananchi wawe 'aware' na kujua nani ni mhamiaji haramu jambo litakalosaidia kupata taarifa za wahamiaji haramu hao na kuweza kuwashughulikia kisheria. Katika mabango na vipeperushi tumeweka namba za simu ambazo zitatumiwa na wananchi kuwasiliana nasi pale wanapomuona au kuwaona wahamiaji haramu mahali popote mkoani, nasi hatutasita kwenda kuwakamata" 
 
 alifafanua Naibu Kamishna Kombe.

"Mabango na Vipeperushi hivi tumeandaa wenyewe hapa ofisini kwetu, tutasambaza vituoni na ofisini za wilaya pamoja na vijiji vya mipakani. Tumepanga kuwa kampeni hii iwe ya kudumu ambayo tunaiita 'UHAMIAJI SHIRIKISHI' ambapo wananchi wenyewe ndiyo wawe watoa taarifa badala ya sasa kuwa wao ndio wanaowahifadhi. Pamoja na changamoto nyingi zitakazojitokeza, hatutakata tamaa, najua kwamba kuna baadhi ya wananchi wana mahusiano ya kijamii na kiuchumi na wahamiaji hawa lakini 'eventually' watakuja kushirikiana nasi tu''
 
alimaliza kueleza kamanda huyo.

Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya wahamiaji haramu nchini ambapo inakadiriwa kwamba kuna zaidi ya wahamiaji 35,000 mkoani hapa kutoka nchi jirani wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki. Madhara ya kuwepo kwa wahamiaji haramu nchini ni pamoja na kukosekana kwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo, serikali kuingia gharama kubwa kuhudumia watu wasiostahili, upungufu wa ajira katika viwanda na sekta nyingine za kiuchumi, na kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu kwani wahamiaji hao huingia na silaha nzito ambazo huzitumia kufanyia vitendo vya uporaji na ujambazi.

Blogu ya Bugango inapongeza idara hiyo mkoani Kagera kwa kuanzisha kampeni hii.

No comments:

Post a Comment