Tuesday 20 August 2013

Rwanda yamchimba Salma Kikwete .....

Mlima Kilimanjaro




Rwanda yamchimba Salma Kikwete



MSIGANO wa kauli baina ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda, unazidi kuchukua sura mpya ambapo sasa vyombo vya habari vya Rwanda vimeanza kuichafua familia ya Rais Kikwete, Mtanzania Jumatano limebaini.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda, vimeanza kuuhusisha ushauri wa Rais Kikwete kwa Rais Kagame wa kumtaka awe tayari kukaa meza moja na waasi wa kundi la FDLR wanaopigana na Serikali ya Rwanda kutoka Mashariki ya Kongo, kuwa msingi wake unatokana na undugu uliopo kati ya mke wake, Mama Salma Kikwete na wabaya wa Kagame.

Wabaya wa Kagame ambao wanatajwa kuwa na undugu wa damu na Mama Salma Kikwete ni Wahutu ambao ni wapinzani wa serikali ya sasa ya Rwanda.

Mtandao wa Rwandanews ambao ni maarufu nchini humo, umeandika kuwa hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Kikwete kugeuka kuwa kiongozi pekee duniani anayewaonea huruma waasi wa kundi la FDLR wa mashariki mwa Kongo tangu mwaka 1994.

Ukizinukuu taarifa za siri zinazodaiwa kuvujishwa na Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwenye mtandao wa Wikileaks, mtandao huo ulidai kuwa mke wa Rais Kikwete, Mama Salma ni binamu wa Kiongozi wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana.

Habyarimana ambaye kwa kabila ni Mhutu, alikuwa Rais wa pili wa Rwanda, aliyeuawa mwaka 1994 baada ya ndege aliyokuwa amepanda kutunguliwa.

Sababu za kutunguliwa kwa ndege yake hazijulikani, ingawa jina la Rais Kagame limekuwa likitajwa kuhusika kwa sababu za kutaka madaraka kwa kutumia ukabila.

Kwa mujibu wa mtandao huo wa Rwandanews, taarifa za Mama Salma kuhusishwa na Habyarimana, zilibainika baada ya kurushwa kwenye mtandao huo Mei 5, 2005 na mtu aliyetajwa kwa jina la Shabyna Stillman, ambaye ni Mwanadiplomasia mwandamizi katika Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam.

Wakati taarifa hizo zikitumwa kwenye mtandao, inasemekana ubalozi wa Marekani ulikuwa ukitoa taarifa juu ya uteuzi wa Kikwete kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi wa rais mwishoni mwa mwaka huo.

Ukinukuu kile ilichodai kuwa ni sehemu ya taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao huo wa Wikileaks, uliandika;

“Kwa miaka mingi, waangalizi wa migogoro ya Maziwa Makuu wamekuwa wakimchukulia Kikwete kwamba anawaunga mkono Wahutu.”

“Kikwete kuoa binamu wa Rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana pengine huenda ikawa kumechochea fununu hizi, ambazo zimekuwa kama upepo uliozima mgogoro wa Burundi,” inaeleza sehemu ya taarifa ya mtandao huo.

Chombo hicho cha habari kilidai kuwa mapenzi ya Kikwete na Wahutu yanaweza kuonekana wazi wakati akiwaunga mkono waasi wa Burundi, walipokuwa wakipambana na Rais wa zamani Pierre Buyoya.

Kwamba tangu mwaka 1995 hadi 2005 wakati Rais Kikwete alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, amekuwa mstari wa mbele kuwatetea waasi hao.

Hata hivyo wakati kukiwa na maswali kuhusu uhalisia wa suala hilo, Mama Salma Kikwete ambaye ni mwenyeji wa maeneo ya Kusini, hajawahi kulizungumza wala kulitolea ufafanuzi wowote.

Lakini kuibuka kwa taarifa hizi wakati huu, kunachochewa na msigano wa kauli, uliojitokeza kati ya Rais Kikwete na Kagame,

Siku chache baada ya Rais Kikwete kumpa ushauri wa kukaa meza moja na waasi wa FDLR, Kagame alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Rwanda akimkejeli Kikwete hata kufikia hatua ya kutoa kauli zenye mwelekeo wa vitisho dhidi yake.

 



Kauli hizo za Kagame zilisababisha Rais Kikwete, kupitia katika hotuba yake mwishoni mwa mwezi Julai, kujibu mashambulizi huku akieleza bayana kushangazwa na kushtushwa na kejeli na matusi yaliyokuwa yakielekezwa kwake.

Akitumia maneno ya kidiplomasia ambayo yametafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya diplomasia na sayansi ya siasa kuwa yanabeba ujumbe mzito, Rais Kikwete alisema alikuwa amesikia yote yanayosemwa kutoka Rwanda na alikuwa hakusudii kuyapuuza.

Wakati hali ikiendelea kuwa ni ya mashaka na kutoaminiana kati ya Tanzania na Rwanda, wiki iliyopita Mtanzania Jumatano, lilikuwa na habari kubwa yenye kichwa cha habari kisemacho; ‘Nini kinamtia Jeuri Kagame?’ ambayo pamoja na mambo mengine, ilieleza namna kiongozi huyo anavyopatiwa baadhi ya taarifa zisizo za kweli na watu wenye asili ya Rwanda waliojipenyeza katika taasisi mbalimbali nyeti za umma.

Taarifa zilizolifikia gazeti muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni zinaeleza kuwa Serikali ya Tanzania imekanusha madai hayo.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, Assah Mwambene, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa taarifa zilizoandikwa kwenye mtandao wa “twitter” na Wanyarwanda kuwa Rais Kikwete ni shemeji wa aliyekuwa Rais wa Rwanda, Havyarimana hazina ukweli wowote.


BOSHAZI....Blog

No comments:

Post a Comment