Thursday 15 August 2013

LEMBELI : VIGOGO SERIKALINI NI MAJANGILINI

LEMBELI :
 
 
 VIGOGO SERIKALINI NI MAJANGILINI


SILAHA


Kamati ya Bunge ya Ardhi,
 Maliasili na Mazingira imesema vigogo wakubwa wa serikali wanaongoza kwa kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu ndiyo maana zoezi la kuzuia majangili halifanikiwi kwa miaka mingi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa James Lembeli (MB), alitoa kauli hiyo ijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Kamati yake kumaliza kikao katika ofisi ndogo za Bunge na kusema kuwa wabunge wamepiga kelele kwa muda mrefu kuhusu tatizo la ujangili wa kuua tembo, lakini serikali inawapuuza kwa kuwa vigogo wake ndiyo wanaohusika.

Mheshimiwa Lembeli alisema vyombo vya dola navyo watumishi wake wanahusika kwa kuwa wanaona wakubwa wao ambao ni vigogo wa serikali wanafanya biashara hiyo haramu ambayo inazidi kuangamiza tembo kila mwaka.

Lembeli alitanabahisha kuwa Kamati yake mara kadhaa imekuwa ikishauri namna ya kukabiliana na vitendo vya ujangili wa kuua tembo, lakini serikali imekuwa haichukui hatua na kwamba baadhi ya bandari ikiwamo ya Dar es Salaam zinatumika kusafirisha meno ya tembo.

Aliongeza kuwa mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete alitembelea Wizara ya Maliasili na Utalii na kuwauliza kama wanahitaji awaongezee nguvu ili kupambana na ujangili, lakini wao mpaka sasa wamekaa kimya hawajasema kama wameshindwa ili wapatiwe msaada.

Majangili wanatumia silaha nzito na maboga kwa kuyaweka sumu na tembo anapokula humchukua dakika 20 kupoteza uhai na hapo majangili hao huchukua meno yao. Meno ya tembo hutengenezea vitu vya urembo kama pete, bangili, mikufu na vitu hivyo huvaliwa na watu wakubwa kama wafalme na malkia.

Hivi karibuni, baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola wakiwamo askari polisi na wanajeshi wamekuwa wakikamatwa na meno ya tembo matukio ambayo yanaelezwa kuwa ni hatari kwa kuwa wao ndiyo walinzi wa usalama na maliasili za taifa.

No comments:

Post a Comment