Sunday 11 August 2013

JAPAN YAICHAGUA TANZANIA KUWA KITOVU CHA BIASHARA AFRIKA

 
JAPAN YAICHAGUA TANZANIA KUWA
 KITOVU CHA BIASHARA AFRIKA
 
 
- Kuboresha reli ya kati, bandari ya Dar na kujenga viwanda

Japan imeichagua Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika, ili kuiwezesha kuwa na uchumi imara na wenye uwezo kuondoa umaskini na kuongeza fursa za ajira.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana, ilisema katika kufikia azma hiyo, Japan itasaidia kuboresha reli ya kati, kuipanua bandari ya Dar es Salaam iwe ya kisasa na kujenga viwanda vikiwamo vya kutengeneza pikipiki za Honda.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania itapata fursa ya kuwa mshirika wa kwanza wa Japan, ikiwa ni matokeo ya mazungumzo baina ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe yaliyofanyika Tokyo Juni, mwaka huu.

Uamuzi huo wa Japan, ulitangazwa rasmi jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo, Toshimistu Motegi, alipozungumza na Rais Kikwete. Motegi, alisema Japan itawatumia wataalamu wake kuiboresha reli ya kati kwa kujenga njia ya kimataifa itakayokuwa mbadala wa reli nyembamba iliyopo sasa.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Motegi ameambatana na wafanyabiashara wa Japan watakaokutana na wale wa ndani, ikiwa ni moja ya mkakati wa kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika Afrika kwenye uwekezaji na uchumi ulioimarika.
Waziri huyo pia alisema Japan imekusudia kuhakikisha bidhaa ambazo zinanunuliwa kutoka Japan, zinazalishwa hapa nchini kwenye viwanda vitakavyojengwa na kampuni za nchini humo.
Alisema, kampuni mbili za Honda na Panasonic zitajenga viwanda vya kutengeneza pikipiki za Honda na kuzalisha vifaa vya umeme.
Pia, alisema kadhalika kampuni za Japan zitawekeza kwenye kilimo hasa cha pamba na kuanzisha viwanda vya nguo.

Akiwa Tokyo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Mkuu, Abe kuwekeza zaidi barani Afrika akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa makubwa duniani ambayo yamefanikiwa kupata soko Afrika hasa eneo la magari.

No comments:

Post a Comment