Tuesday, 2 July 2013

WATANZANIA WAJITOKEZA MABARABARANI kumuaga Rais Obama


WATANZANIA WAJITOKEZA MABARABARANI kumuaga Rais Obama


Dar es Salaam. Rais wa Marekani Barack Obama amehitimisha ziara yake ya Afrika mapema leo, kwa kutembelea mradi wa uzalishaji umeme wa Symbion Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake Ubungo, Rais Obama alielezea jinsi mkakati wa serikali yake wa kuhakikisha Afrika inapata umeme utakavyoboresha maisha ya wakazi wa bara hili.
Mapema leo asubuhi, Rais Obama aliungana na Rais wa zamani wa Marekani George Bush kuweka shada la maua kuwakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi la ubalozi wa Marekani mwaka 1998.
Katika ziara yake ya siku mbili iliyoanza jana nchini Tanzania, Rais Obama amesisitiza umuhimu wa kuboshesha mahusiano ya kibiashara kati ya Afrika na Marekani.
Wakati wa ziara yake, Obama aliahidi kutilia mkazo vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania.
Marekani itaisaidia serikali ya Kikwete kuboresha miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za kielimu kwa  vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Jijini Dar es salama, Barabara za Ally Hassan Mwinyi, Mandela, Sam Nujoma na ile ya Morogoro zilifungwa kwa muda kuanzia majira ya saa tatu asubuhi huku maelfu ya wananchi wakitanda barabarani kwa lengo la kumuaga rais huyo.
Mara baada ya kufika katika  uwanja wa Ndege Rais Obama na Mkewe walitumia  muda mfupi kuagana na mwenyeji wao Rais Kikwete na mkewe ikiwa ni pamoja na kuwaaga mamia ya viongozi waliofika uwanjani hapo.
Mikakati ya Marekani Afrika
Kiongozi huyo aliwasili Dar es Salaam jana mchana ikiwa ni nchi ya mwisho katika ziara yake barani Afrika ikitanguliwa na Senegal na Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Rais Obama alisema aliainisha mambo hayo wakati alipozungumza na mwenyeji wake huyo.
Alisema katika mazungumzo hayo, waligusia mradi wa mkubwa wa umeme uitwao Power Afrika wenye lengo la kuongeza kiwango cha umeme kinachozalishwa nchini na barani Afrika ili kupata umeme nafuu na wa uhakika utakaochagiza kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.
Nchi nyingine za Afrika ambazo zitanufaika na mpango huo ni Kenya, Ghana, Liberia, Nigeria na Ethiopia.
Rais Obama alisema pia wamezungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo, ukuzaji wa demokrasia na utawala bora.
Alimzungumzia pia mchezaji nyota wa mpira wa kikapu wa Tanzania, Hashimu Thabeet anayecheza katika Ligi Kuu ya Marekani (NBA), akiwa na timu ya Oklahoma Thunder ya Marekani, akisema hawakuzungumzia suala lake na kuahidi kufanya hivyo siku nyingine.
Akijibu swali iwapo anaridhishwa na misaada ambayo nchi yake inatoa kwa Tanzania, Rais Obama alisema anafarijika kwa matunda yanayopatikana katika mapambano dhidi ya malaria, barabara mpya zinazojengwa na katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Hatutoi dawa, bali tunajenga miundombinu ya afya, hatutoi chakula, bali kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula pia tunasisitiza kubadilishwa kwa sheria mbalimbali ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kuleta mitaji yao kwa wingi zaidi, lakini jambo la muhimu ni kuijenga Afrika,” alisema.
Kuhusu sekta ya utalii, Rais Obama alisema watatangaza vivutio vya Tanzania, lakini kwa kuwa ameambiwa ujangili ni tatizo, Serikali yake itaisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tutatangaza utalii, nimeelezwa ujangili ni tatizo hivyo Marekani itasaidia kupambana na changamoto hiyo na tutaongeza fedha kuhakikisha hali hiyo inatokomea,” alisema.
Akichangia hoja ya misaada ya Marekani, Rais Kikwete alisema Mradi wa Maendeleo ya Changamoto za Milenia (MCC), umekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania.
Alisema kupitia MCC, Tanzania imepata msaada wa kujengewa barabara katika maeneo ya vijijini na yale yanayozalisha chakula kwa wingi.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamenufaika kwa barabara hizo kuwa ni Namtumbo, Songea, Mbinga, Tunduma, Horohoro, Tanga  na baadhi katika Kisiwa cha Pemba.
Alisema Tanzania pia imenufaika kwa mradi wa maji jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake unaendelea na umeme kwa ajili ya maeneo ya vijijini ambao pia unafadhiliwa na Marekani katika mikoa 10 ya Tanzania.
“Kusema kweli Marekani imefanya makubwa, nikisema inatosha, Mheshimiwa Rais hatasikiliza maombi yangu mengine,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kutokana na misaada ya Marekani, maambukizo ya Ukimwi yamepungua, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua na wale wanaozaliwa na wakiwa na VVU wamepungua kwa kiwango kikubwa.
Alisema pia Watanzania wamenufaika na msaada wa vitabu milioni mbili vya sayansi. Alitumia fursa hiyo kuomba idadi nyingine kama hiyo.
“Nimemwambia tunaomba vitabu vingine milioni mbili na yeye akasema niongee na watu wake, lakini nilipowatazama nikaona nyuso zao zinakubaliana na Rais wao,” alisema Kikwete.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliulizwa kuhusu kesi ya Mtanzania aliyeshtakiwa Marekani kwa kumtumikisha binti wa Kitanzania na kushindwa kulipa faini na kusema analifahamu suala hilo, lakini limemalizika kwa wahusika kulipwa.
Alisema binti aliyelalamika alichukuliwa na dada yake kwenda kusomeshwa Marekani, lakini alipofika akatumikishwa kwa kazi za ndani aliwashtaki dada yake na shemeji yake na mahakama ikawatoza faini ya Dola milioni moja za Marekani.
Hata hivyo, alisema haikuwa rahisi kwa wadaiwa kulipa faini hiyo kutokana uwezo wao mdogo, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, hivyo waliomba faini ipunguzwe na ilipopunguzwa ikalipwa na suala hilo likamalizika.
Aimwagia Tanzania Sifa
Akiizungumzia Tanzania, Obama alisema, “Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Tanzania, mzee wangu alikuwa Afrika Mashariki na wakati fulani aliishi Tanzania, mke wangu na watoto wangu wamefurahi kufika hapa.”
Alisema alipoingia madarakani Rais wa kwanza kutoka Afrika kukutana naye alikuwa ni Rais Kikwete kwa kuwa Tanzania inaheshimu utawala wa kidemokrasia.
Obama alisema Tanzania imefanya kazi nzuri pamoja na Zanzibar kwa kufanikisha suala la Katiba Mpya kwa ajili ya Tanzania ijayo kwani hiyo ndiyo demokrasia.
Pia aliipongeza Tanzania kuhusu hatua yake katika kulinda amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Sudan hasa eneo la Darfur.
Alisema DRC inaathiriwa na machafuko kutokana na kuwa na maliasili nyingi na kusema Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila na watu wake wanahitaji kufanya kazi kubwa kuhakikisha amani inakuwapo.

No comments:

Post a Comment