Walioiba fedha ujio wa
marais wabanwe
Kama kuna jambo ambalo linamshangaza kila mgeni anayetembelea nchi yetu, jambo hilo ni umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi, huku nchi ikiwa na utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali za kila aina pengine kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika.
Wananchi wengi pia wamekuwa wakitatizwa na hali
hiyo, hivyo kuuliza maswali mengi pasipo kupata majibu. Lakini jambo
moja ambalo wananchi wengi wamelibaini kama moja ya sababu kubwa za
kuwapo umaskini wa kutisha nchini ni kuporomoka kwa maadili ya viongozi
na kupotea kwa uzalendo.
Ni vitendo hivyo ambavyo vimetuletea laana na
kudidimiza uchumi wa nchi. Baya zaidi ni pale wengi wa wale waliopewa
dhamana ya kuongoza nchi na kulinda rasilimali zake, ndiyo walewale
wanaowageuka wananchi na kuhujumu uchumi kwa vitendo vya wizi na
ubadhirifu wa rasilimali hizo. Wananchi wameachwa njiapanda wakiwa
katika umaskini wa kutisha na kulazimika kuishi kama wakimbizi katika
nchi yao.
Tumelazimika kusema hayo kutokana na vitendo hivyo
kuendelea kushamiri kiasi kwamba wananchi hawaoni tena kama viongozi
wana uchungu na nchi. Kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samwel Sitta kwamba Sh8 bilioni zilizotumika wakati
wa Mkutano wa Smart Partnership uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi
karibuni zilifujwa na baadhi ya watumishi wa Serikali, ni kauli
inayodhihirisha kwamba nchi yetu sasa ni mateka wa kudumu wa ufisadi na
haina tena matumaini ya kujenga uchumi shirikishi unaotumia rasilimali
za nchi kuwanufaisha wananchi.
Tunampongeza Waziri Sitta kwa kumfunga paka
kengele na kukataa kuficha maovu kwa kisingizio cha uwajibikaji wa
pamoja. Bila shaka kauli yake hiyo itakuwa imewaudhi na kuwafadhaisha
wenzake wengi katika Baraza la Mawaziri ambao wamekuwa wakiona ufisadi
ukifanyika lakini wanafunika kombe ili mwanaharamu apite. Dhana ya
uwajibikaji wa pamoja imekuwa ikipotoshwa makusudi. Viongozi wengi
wametumia dhana hiyo kuficha maovu, hata pale maovu hayo yanapokuwa na
viashiria vya kuiangamiza nchi na watu wake.
Tunakubaliana na Waziri Sitta kwamba ufisadi huo
lazima uchunguzwe na hatua madhubuti na stahiki zichukuliwe.
Tunakubaliana naye pia kwamba CAG ndiye achunguze kashfa hiyo kwa sababu
amejijengea sifa ya uadilifu, hivyo ripoti yake haitegemewi kumlinda
mtu yeyote, wala kuficha jambo lolote chini ya zulia.
Umuhimu wa kauli ya Waziri Sitta ni kwamba
imezionyesha mamlaka husika mahali pa kuanzia. Kwamba fedha hizo
zilifujwa na baadhi ya watumishi wa Serikali ambao walijitengenezea
kampuni bandia za mapambo, machapisho na nyingine ambazo hazijasajiliwa.
Katika hali hiyo, hakuna anayeweza kubisha kwamba watumishi hao
walifanya ufisadi huo kwa baraka na ushirikiano wa vigogo wa ngazi za
juu kabisa katika Serikali.
Serikali ina hali mbaya sana kifedha hivi sasa,
lakini ndio kwanza mafisadi wanazidisha kasi ya kuihujumu. Zipo pia
habari zisizoacha shaka kwamba mabilioni ya fedha pia yalifujwa na
mafisadi serikalini wakati wa mkutano wa Wake za Marais barani Afrika
uliofanyika jijini Dar es Salaam na wakati wa ziara za marais Baraka
Obama wa Marekani na Rais Xi Jinping wa China hapa nchini. Kashfa hiyo
inajulikana vizuri serikalini, lakini mamlaka husika zimekaa kimya
pengine kwa kisingizio cha uwajibikaji wa pamoja.
No comments:
Post a Comment