Wednesday, 31 July 2013

RAIS ANG'AKA....KAGERA


 Balozi Khamis Kagasheki 





Bukoba. Rais Jakaya Kikwete amewaagiza Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Aman kumaliza mara moja mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kwenye manispaa hiyo ukiwahusisha.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Kagera kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Akihutubia mkutano huo, Rais Kikwete alimtaka Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii kuzungumza mgogoro huo na alipopanda jukwaani alisema miradi iliyopangwa kutekelezwa na Manispaa ya Bukoba chini ya meya huyo haiko wazi, inawaumiza wananchi na ina harufu ya ufisadi.
Alisema kulikuwa na mgawo wa viwanja vilivyokuwa vitolewe kwa wananchi na walikuwa wamelipia fedha kwa ajili hiyo, lakini havikuwahi kutolewa. Alisema kuna viwanja 5,000 lakini havijatolewa mpaka sasa.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema haoni sababu ya wawili hao kuendelea kulumbana na kusema kinachotakiwa ni kukaa pamoja kupima viwanja vilivyopo na utaratibu wa kugawa uendelee.
“Ugawaji viwanja uendelee, kila mwenye kustahili apewe na ambaye hakuridhika ana nafasi ya kukata rufani... hakuna sababu ya kuendelea kulumbana,” alisema Rais.
Mgogoro kati ya Meya Amani na Balozi Kagasheki, ulianza baada ya Manispaa ya Bukoba kuanza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa soko la kisasa, kituo cha mabasi na upimaji wa viwanja 5,000.
Mapema Machi mwaka huu, CCM, kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kilitolea tamko mgogoro huo na kusema hauna tija na badala yake, unarudisha nyuma jitihada za kuimarisha chama.
Nnauye, aliwataka wakazi wa Manispaa ya Bukoba  kuendelea na shughuli zao zikiwamo za miradi ya maendeleo.
Atembelea mpaka wa Tanzania na Rwanda
Akihutubia umati wa wanaCCM, Rais Kikwete alirejea hotuba yake ya Siku ya Mashujaa kuhusu atakayeigusa Tanzania: “Watu hawakunielewa, wapo walioanza kufikiria sasa naanza vita, nilichokisema ni kwamba atakayetuchokoza hatutamwacha.
“Siwezi kuagiza jeshi kuvamia nchi, jeshi letu ni kwa ajili ya ulinzi wa amani ya taifa letu, kwa wananchi na mipaka. Sitaruhusu hilo, sasa kama kuna mtu anafikiria vingine, shauri yake.”

Juzi Rais Kikwete alitembelea mpaka wa Tanzania na Rwanda kuona shughuli mbalimbali zinazoendelea katika mpaka huo.
Rais Kikwete alisimama kwa muda ili kukagua ujenzi wa kituo cha kuhudumia shughuli za mpakani kati ya Tanzania na Rwanda eneo la Rusumo, ambacho kukamilika kwake kutapunguza tatizo la kuchelewesha usafirishaji wa mizigo na usafiri wa abiria kati ya nchi hizo mbili.
Alielezwa kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho ambacho kitafanya kazi kwa saa 24, kitapitisha magari kati ya 400 na 500 kwa siku.

No comments:

Post a Comment