Saturday, 27 July 2013

Sudan Kusini

130723195340_south_sudan_304x171_reutersMarekani na Umoja wa Ulaya wamewataka viongozi wa Sudan Kusini kuendeleza hali ya utulivu na kuzuia vitendo vya ghasia baada ya Rais Salva Kiir kulivunja baraza la mawaziri akiwemo naibu wake.
Marekani imesema imesikitishwa sana na hali ya kuhatarisha utulivu wa taifa hilo changa duniani.
Bwana Kiir alilivunja baraza la mawaziri siku mbili zilizopita katika kile kinachoonekana kuwa ni kugombea madaraka kati yake na makamu wa rais Riek Machar.

Sudan Kusini yenye utajiri mkubwa wa mafuta ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011 baada ya miaka mingi ya mgogoro kati ya nchi mbili hizo.
Vikundi mbalimbali vyenye silaha vimeendeleza harakati zao nchini humo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini Mayek Makol amesema Rais Kiir anafanya mashauriano akipanga kuunda serikali mpya.
Hata hivyo amekataa kusema mashauriano hayo yatachukua muda gani.
“huenda yakachukua siku tatu, nne, au wiki moja”, amesema.
Kwa wakati huu wafanyakazi waandamizi wa umma, wanaendesha shughuli za serikali ya nchi hiyo ambayo ni ya mwisho kwa maendeleo duniani.
Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema:” Ni muhimu kwa Sudan Kusini kubaki na mtazamo wake wa ukweli iliouonyesha wakati wa siku ya uhuru wake miaka miwili iliyopita.”
Zaidi ya watu milioni 1.5 waliuawa na wengine zaidi ya milioni nne kukosa mahali pa kuishi wakati wa mgogoro kati ya Sudan Kusini, ambako watu wengi ni Wakristo au kufuata imani za dini za kimila, na waislam wenye kuzungumza Kiarabu , Sudan kaskazini.
Lakini nchi hiyo imepata matatizo sugu ya kiuchumi tangu wakati huo na kuimarika kwa uchumi wake kumecheleweshwa na mvutano juu ya mpaka na mafuta kati yake na majirani zao Sudan Khartoum.

No comments:

Post a Comment