Wamiliki kampuni za simu
wataka ufafanuzi TRA
Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Simu nchini (Moat), kimeitaka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuvitolea ufafanuzi baadhi ya vifungu vilivyoko kwenye Sheria ya Fedha ya mwaka 2013.
Katika barua yao kwa Kamishna Mkuu wa TRA nchini, Harry Kitilya, ya Julai 5 mwaka huu, walisema wasiwasi wao kwenye vifungu hivyo upo kwenye vipengele vya matumizi sahihi na iwapo vitaweza kutekelezeka.
Kwa mujibu wa barua hiyo, changamoto wanayokabiliwa nayo ipo pia kwenye ugumu wa kutekelezeka kwa marekebisho hayo ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 hasa kwenye vifungu vya 124 (3), vya Sheria ya ushuru wa bidhaa na Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.
Baadhi ya vifungu ambavyo Moat, waliviorodhesha ili viweze kuangaliwa upya na TRA ni pamoja na kile cha huduma za fedha za simu na ushuru wa bidhaa wa asilimia 0.15 kwa kiasi cha kuhamisha fedha zaidi ya Sh.30,000, kwa madai ya kwamba sheria hiyo ya fedha haijafafanua maana ya kuhamisha fedha.
Kifungu kingine ni kile cha ushuru wa fedha kuhusu huduma ya uunganishaji na uhamishaji na kwamba changamoto iliyopo ni kuongezeka kwa kodi mara dufu kwa mawasiliano ya simu ya ndani na nje ya nchi.
Athari ya kiuchumi katika kipengele hicho ni kuongezeka kwa viwango kwa wamiliki wa nje ili kufidia ushuru wa bidhaa usiotosheleza.
Kifungu kingine kwenye sheria hiyo ni kile cha ushuru wa bidhaa kwenye laini ya simu (sim card), ambacho kinaeleza kuwa, kutakuwa na tozo ya kodi ya kiasi cha Sh.1,000 katika laini ya mawasiliano ya simu kila mwezi.
Kuhusiana na hilo, Moat wanaitaka TRA kutoa ufafanuzi kwenye kifungu hicho kwa hoja ya kwamba kinahusika na laini za simu zilizosajiliwa tu au na zile ambazo hazijasajiliwa.
Pia walitaka ufafanuzi wa msingi wa kutambua laini inayotumika katika kujua pia salio la kupiga simu, shughuli na idadi ya miito iliyopokelewa au iliyotoka.
Hata hivyo, Moat waliitaka TRA kutoa ufafanuzi kwenye kipengele cha zuio kutokana na ada ya huduma kwamba maana ya huduma haieleweki vizuri na inahitaji kufafanuliwa vyema ili kuepuka mkanganyiko.
Hoja hiyo ni moja ya zile zilizoainishwa na Moat kwenye Kifungu cha 27 (c) (iii) cha sheria hiyo ya fedha ambacho kimeweka asilimia tano ya kodi ya zuio (WHT) kama ada ya huduma katika malipo kwa wateja.
Barua hiyo ya Moat pia imenakiliwa kwa Wizara ya Fedha na Uchumi, TRA, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) pamoja na kampuni za simu za Airtel, Vodacom, Tigo, Zantel na TTCL.
Hivi karibuni kampuni za simu za mkononi nchini pamoja na viongozi mbalimbali wakiwamo wa vyama vya siasa, walipinga kipengele hicho cha kodi kwa kila laini ya simu kwa watumiaji wa mitandao hiyo na kupelekea Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, kuueleza umma kwamba wameyapokea na watayafanyia kazi
No comments:
Post a Comment