Saturday, 20 July 2013

MAGALI YA MABOMBA YAGESI...MTWARA




Gari la mabomba gesi 

ladaiwa kurushiwa jiwe





Gari lililokuwa likisafirisha mabomba ya gesi kutoka Mtwara kwenda Lindi, limedaiwa kurushiwa jiwe na mtu asiyejulikana na kusababisha kioo cha mbele kuvunjika.
Tukio hilo limetokea eneo la kijiji cha Msijute, Wilaya ya Mtwara Vijijini. Gari lililopata mkasa huo ni lenye namba za usajili T 164, CLV aina ya Cheng LONG, lililokuwa likiendeshwa na Said Mohamed ( 31).
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini alisema ilikuwa ni ajali iliyosababishwa na basi lililokuwa likipishana na gari hilo, lenye namba za usajili T 178 ASU, aina ya Scania, kukanyaga jiwe na kurukia kwenye kioo cha gari hilo.
Alimtaja dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo kuwa ni Mwalimu Mbwana (27), mkazi wa Kigogo, jijini Dar es Salaam.
Alisema gari lililovunjika kioo lilikuwa likisafirisha mabomba ya kutekeleza mradi wa usafirishaji wa gesi asilia inayotoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa njia ya bomba.
Alisema tukio hilo lilitokea jana, majira ya saa 9:45 alasiri, ambapo basi hilo lilikanyaga jiwe na kurukia kwenye kioo cha mbele, wakati yanapishana.

“Gari hilo baada ya kupasuka kioo lilishindwa kuendelea na safari, kutokana na tatizo hilo uchunguzi unaendelea ili kubaini tatizo hilo,” alisema. Kwa mujibu wa Kamanda Sinzumwa, hakuna

mtu yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Hata hivyo, habari zaidi kutoka chanzo chetu cha habari, zinadai kuwa, baada ya tukio hilo, basi hilo lilikamatwa na kupelekwa Kituo kikuu cha polisi Mtwara.
“Baada ya ajali hiyo basi lilikamatwa na kupelekwa kituoni, na baada ya hapo askari walilazimisha abiria kumtaja mtu aliyerusha jiwe hilo,” alidai mmoja wa abiria aliyekuwa ndani ya basi hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Chanzo hicho kilisema kuwa baada ya abiria kushindwa kumtaja mtu anayedaiwa kurusha jiwe hilo, abiria waliwekwa kituoni hapo mpaka saa 2 usiku juzi.

“Abiria wote walikaa kituoni hapo mpaka saa mbili usiku, hakuna abiria aliyeruhusiwa kwenda kula, akina mama na watoto wote walikaa mpaka muda huo,”

 kilieleza chanzo hicho.
Gari hilo lililokuwa likisafirisha mabomba hayo kwenda mkoani Lindi katika kijiji cha Kiranjeranje, lilikuwa likisindikizwa na askari aliyetambulika kwa jina moja la Meja Frank.
Uzinduzi wa mabomba ya ujenzi wa gesi ulizinduliwa rasmi juzi katika Bandari ya Mtwara, na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na viongozi mbalimbali, akiwamo Balozi wa China nchi Tanzania.
Shehena ya kwanza ya mabomba 4,600, ilipokelewa ambapo ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza Agosti mosi, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment