Saturday, 27 July 2013

Urani kuingizia Taifa 

Sh trilioni 2


uranium

Urani kuingizia Taifa pato kubwa

SERIKALI inatarajia kuingiza kiasi cha Sh trilioni 1.6 kutokana na uwekezaji katika mradi wa uchimbaji urani wa Mkuju wilayani Namtumbo, Ruvuma. Mradi huo unaotarajiwa kuanza mwaka 2016 unamilikiwa na Mantra Tanzania na kuendeshwa na Uranium One Inc.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Uranium One, Chris Sattler, mradi huo utafuata viwango vya kimataifa vya Shirika la Kimataifa la Atomiki, vya nchi na kanda.
“Kama ilivyo kwa miradi mingine ya urani duniani, huu wa Mkuju utazingatia viwango vyote vya usalama,” Sattler alisema wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya usalama wa mradi huo hivi karibuni. Mwaka jana, Tanzania ilipata idhini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kurekebisha kwa kiwango kidogo mipaka ya mbuga ya Selous katika sehemu ambako mradi huo utatekelezwa.

Satter akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra Tanzania, Asa Mwaipopo, alisema utekelezaji wa mradi huo kwa sasa unasubiri idhini mbili kutoka serikalini.
“Kinachosubiriwa sasa ni kutia saini na Serikali katika mkataba wa uendelezaji wa uchimbaji madini (MDA) kwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini. Vilevile, tutahitaji idhini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili mradi uanze,” alifafanua.
Mradi utakapoanza, urani itakayochimbwa itatumika kufua umeme kwa nguvu za nyuklia nchini na nchi nyingine zilizowekeana saini ya matumizi sahihi ya nishati hiyo, alibainisha.
Tanzania inatarajiwa kuwa nchi ya tatu Afrika kwa uzalishaji wa urani baada ya Niger na Namibia. Kwa mujibu wa Mwaipopo, wataajiriwa wafanyakazi 1,600 wakati wa ujenzi wa mgodi na wengine 700 mradi utakapoanza kazi.

“Kwa sasa kuna wafanyakazi 120 ambao wanahusika na utafiti,” Mwaipopo alisema. Mjiolojia Mwandamizi katika mradi huo, James Magweiga, aliwaambia waandishi wa habari kwamba hadi Novemba mwaka jana, utafiti ulionesha kuwapo tani 54,000 za urani.

“Kwa kiwango hiki, tunatarajia mgodi uzalishe kati ya miaka 12 na 15. Hata hivyo utafiti bado unaendelea kuona kama kuna kiwango zaidi cha urani,” mtaalamu huyo alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Abdula Lutavi, alisema wananchi wa Namtumbo wana shauku kubwa na mradi huo katika kufungua fursa za biashara na uwekezaji.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alizindua machinjio ya kisasa Namtumbo ambayo yatatumika pamoja na mambo mengine, kuchinja wanyama watakaouzwa katika mradi wa Mkuju.

No comments:

Post a Comment