Jarida la kimataifa lawatuhumu
vigogo kuhujumu
sera ya dawa
Dar es Salaam. Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la kimataifa unaonyesha kuwa mchakato wa mabadiliko ya sera ya uuzaji wa dawa za binadamu nchini, umegubikwa na ufisadi ukihusisha viongozi wa Serikali.
Jarida la Afya la Kimataifa linalochapishiwa
nchini Uingereza, limechapisha utafiti huo likisema mabadiliko ya sera
hiyo ambayo sasa imebadili mfumo uliokuwapo wa maduka ya dawa baridi za
binadamu, kuwa ya dawa muhimu sasa ni janga linalozinyemelea afya za
Watanzania.
Kwa mujibu wa jarida hilo hadi upitishwaji wa
muswadwa wake bungeni, uliingiliwa na vigogo serikalini pamoja na
wafanyabiashara wakubwa kwa malengo ya kujinufaisha.
Jarida hilo linaloitwa BMC Public Health toleo la
mwezi huu, limechapisha ripoti hiyo wakati ambapo tayari Serikali
imeanza kutekeleza sera hiyo kwa kubadili maduka ya dawa baridi kuwa
maduka ya dawa muhimu ambapo yanatatawanywa hadi vijijini na
yataruhusiwa kuuza baadhi ya dawa kali za magonjwa makubwa.
Hata hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imetoa msimamo wake ikisema inaichukulia ripoti hiyo kama ni maoni
ambayo mtu yeyote anaweza akayatoa, na kwamba hawatarudi nyuma kwa kuwa
wanajiamini mchakato ulifuata sheria na taratibu za nchi.
Yaliyomo kwenye ripoti
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa utafiti ulifanyika
kati ya mwaka 2011 na 2012, na kubaini kuwa kuundwa kwa sera hiyo,
kulizingatia zaidi masilahi binafsi yaliyoandamana na msukumo wa kisiasa
na kibinafsi.
Inaeleza sera hiyo haikuzingatia ufanisi wa
kitaalamu wa huduma nzuri katika sekta ya afya bali kuweka wigo mpana
ambao mtu yeyote mwenye fedha au anayeshawishika na biashara hiyo aweze
kuwekeza bila kipingamizi.
Jarida hilo liliipa ripoti hiyo kichwa cha habari:
“Mabadiliko ya sera kisekta: Ni kwa ajili ya ufanisi au kuweka wigo
mpana ili kila anayevutiwa awekeze? Ni ripoti ya utafiti uliofanyika
Tanzania kuhusu mabadiliko ya sera ya uuzaji wa dawa.”
Jambo hilo likatafsiriwa kuwa ni la hatari na
ambalo Serikali inapaswa kuingilia kati ili kuepusha janga la kiafya
linaloinyemelea jamii.
“Serikali inapaswa kuingilia kati na kupunguza
ushawishi wa kisiasa kwa masilahi binafsi kwenye mambo ya kitaaluma,”
inashauri sehemu ya taarifa hiyo ikionya:
“Kutoondoa tatizo hilo la udhibiti wa dawa kunaweza kusababisha madhara makubwa ya afya kwa umma.”
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ilisimamiwa na wataalamu watatu wa afya; Amani Thomas Mori, Eliangiringa Amos Kaale na Peter Risha.
Inaeleza mchakato wa kuunda sera hiyo una kasoro
kuanzia uundaji wa kamati, mijadala hadi upitishwaji wa muswada huo
bungeni ili kuwa sheria.
Ilielezwa kuwa mfumo mzima ulitawaliwa na ubabe wa
uamuzi, ambao wadau ama hawakuhusishwa au walijikuta wanakwepwa kwenye
hatua ya kuamua au kufanya majumuisho.
Kwa namna sera hiyo mpya ilivyo, inaelezewa kuwa
inaruhusu ushindani wa kibiashara unaoweza kuathiri baadhi ya
wawekezaji, hivyo kujenga mazingira ya kuendesha biashara hiyo kwa
ujanja jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa dawa.
Utafiti huo uliofanyika kwa mahojiano na watu
mbalimbali unaeleza kuwa baadhi ya wafamasia hawakuridhika na mchakato
wa kuunda sera hiyo, kwa sababu ulizingatia maoni na mapendekezo ya watu
wengi nje ya fani hiyo ya kifamasia.
Kasoro nyingine inaelezwa baadhi ya watu wasio wa
fani hiyo walijipigia kampeni ili wawepo kwenye kamati za kujadili sera
na kuna wajumbe wengine nao walishawishiwa ili washiriki bila kuzingatia
wako kwenye fani ya dawa au la.
Ripoti hiyo inasema licha ya muswada huo kupata
upinzani mkali bungeni, ulipitishwa mabadiliko ya sera ya maduka ya dawa
ya mwaka 2011, kifungu cha nne kinachoruhusu usajili wa maeneo na
maduka ya dawa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) ilipewa mamlaka ya kutoa vibali kwa viwanda vya dawa na
biashara za jumla, huku Baraza la Famasia ambalo ndilo linasimamia
taaluma ya dawa likiachwa katika kusajili biashara za dawa za rejareja.
Mbaya zaidi wakati wa kupitishwa kwa muswada
walikwenda baadhi ya watu kuwahamasisha wabunge waukubali ili upite,
jambo ambalo watafiti hao wanahoji kulikuwa na sababu gani ya kufanya
hivyo kama sera iliandaliwa vizuri.
Kauli ya Serikali
Gazeti hili lilipowasiliana na Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kuhusiana na suala hilo, Ofisi ya Habari na Mawasiliano
Kwa Umma ilisema kuwa msimamo wa Serikali ni kwamba mchakato wa
mabadiliko ya sera ya uuzwaji wa dawa nchini yalizingatia taratibu zote
za kuwahusisha wadau.
Msemaji huyo wa Wizara, Nsachris Mwamaja alisema
kwenye mchakato huo hakukuwa na ushawishi na kwamba waliotoa utafiti huo
walizingatia zaidi maoni yao.
“Sisi tunachukulia ripoti hiyo kama ni maoni waliyotoa wao, kama
ambavyo mtu yeyote anaweza akatoa maoni yake kuhusu jambo hilo. Hakuna
mtu anayezuiwa,” alisema Mwamaja akisistiza:
“Ninachosema ni msimamo wa Wizara. Mchakato wote
uliendeshwa kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi na tunaamini
utakuwa na manufaa kwa wananchi.”
Alipoulizwa kuhusu TFDA kuwa msimamizi wa vibali
vya uzalishaji dawa na ununuzi wa jumla, badala ya Baraza la Mafamasia
ambalo ndilo lenye wataalamu katika fani hiyo alisema:
“Ninachotaka ufahamu ni kwamba hata TFDA wana wataalamu wa dawa. Huo ni utaratibu tu na hakuna jambo linaloharibika.”
Gazeti hili lilipowasiliana na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margaret Sitta alisema
jambo hilo ni nyeti na asingependa kusema chochote kwa sababu hajasoma
ripoti hiyo kwa undani.
Kamati ya Bunge yanena
Hata hivyo, Sitta alisema ripoti hiyo wakiipata
wataijadili kwenye kamati hiyo katika vikao vitakavyoanza mwezi ujao ili
kujua hatua ya kuchukua.
Sakata hilo limekuja wakati ambapo hapa nchini
imebainika kuwa tayari wafanyabiashara hapa nchini wameuza dawa feki za
Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARV).
Tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii imekiri kwamba Kampuni ya TPI Ltd, iliyopo Arusha iliiuzia
Bohari ya Dawa (MSD) ARV aina ya TT-VIR 30 toleo Na.0C.01.85.
Hali hiyo imezusha mtafaruku kiasi cha kusababisha
baadhi ya waathirika kutangaza nia ya kutaka kuishtaki Serikali pamoja
na watengenezaji wa dawa hizo, kwa sababu zinaweza zikawa
zimewasababishia madhara.
Baraza la Famasia
Msajili wa Bodi ya Wafamasia, Mildred Kinyawa
aliwahi kuzungumza na gazeti hili akisema sera ya maduka baridi
ilibadilishwa kuwa ya dawa muhimu baada ya Serikali kubaini kuna uuzaji
na matumizi holela ya dawa nchini. “Tumegundua hilo na ndiyo maana
tumebadilisha mfumo wa maduka ya dawa baridi na kuitwa maduka ya dawa
muhimu,” anasema Kinyawa ambaye ni mtaalamu wa dawa.
Anafafanua: “Uuzaji wa dawa ni biashara lakini ni huduma ambayo
ni regulated (inayofanyika chini ya usimamizi) na Serikali. Siyo kila
mtu anaruhusiwa kuuza dawa.”
Pamoja na msimamo huo, anasema katika miaka ya
nyuma kutokana na kuwapo kwa wataalamu wachache wa dawa Serikali
ililegeza masharti ya uuzaji wa dawa.
Anasema Serikali iliweka kanuni ya mtu yeyote
mwenye akili timamu kuuza dawa baridi, ili mtu yeyote aweze kupata
huduma ya kwanza kama vile kutuliza homa au maumivu.
Kulingana na kanuni mpya, alisema maduka ya dawa
muhimu yatakuwa nje ya miji wakati yatakayoruhusiwa mijini ni yale yenye
wataalamu wa dawa ambayo yatajulikana kwa jina la Famasi.
Sheria mpya ya maduka ya dawa muhimu, anasema yatauza dawa baridi, zikiwepo baadhi moto.