Sunday 8 September 2013

Wanafunzi 868,030 kuhitimu Darasa la Saba....Tanzania



 
Maporomoko ya maji


Dar es Salaam. Wanafunzi 868,030 wa Darasa la Saba wanatarajiwa

kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi Jumatano na Alhamisi wiki hii, ikiwa ni mwanzo wa mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa utakaotekelezwa kwa kuanzia katika mitihani hiyo.
  Taarifa ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), inaonyesha kuwa wanafunzi hao wanatoka kwenye shule 15,677 zikiwamo za umma na binafsi.
  Inaeleza taarifa hiyo kuwa, wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani wa lugha ya Kiswahili ni 844,810  kati yao wasichana wakiwa 444,475 na wavulana 400,335.    Kati ya wanafunzi hao, wasioona ni 88 wavulana wakiwa ni 56 na wasichana 32 huku wenye uono hafifu wakiwa 546 na kati yao wavulana ni 263 na wasichana 283.


  Watakaofanya mtihani huo kwa lugha ya  Kiingereza ni 22,535 na kati yao wavulana wakiwa 11,430  na wasichana 11,105.       Wanafunzi wenye uono hafifu kati ya hao ni 51, wavulana wakiwa 21 na wasichana 30.
 Mwaka jana wanafunzi 894,881 kutoka shule 15,363 walifanya mtihani huo, huku wale waliofanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili wakiwa 873,837 wavulana walikuwa 415,572 na wasichana 458,265.
  Waliofanya  mtihani huo kwa lugha ya Kiingereza walikuwa 20,457  wavulana wakiwa 10,422 na wasichana 10,035. Wenye uono hafifu walikuwa ni 45 wavulana wakiwa 26 na wasichana 19.
 Msemaji wa Necta, John Nchimbi, alilieleza gazeti hili kuwa tayari mitihani imeshasambazwa huku akionya kuhusu wale watakaojaribu kufanya udanganyifu wa aina yoyote ile.
  “Tunawataka wanafunzi na wadau wote wanaohusika na mtihani huu, wasije wakajihusisha na udanganyifu kwa namna yoyote ile, Necta tupo makini na tumejipanga kwa chochote kitakachotokea,” alisema na kuongeza:


 “Tunaamini kuwa wanafunzi wameandaliwa vya kutosha na wao ni vyema wajiandae zaidi kisaikolojia, yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu tutamchukulia hatua zinazostahili ikiwa ni pamoja na kumfutia matokeo.”
 Wanafunzi hawa wanaanza mtihani wakati ambapo Serikali imeweka lengo la kuinua ufaulu wa mtihani huo kutoka asilimia 31 za mwaka jana mpaka 60 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Maandalizi ya mwisho
Shule mbalimbali za msingi zimeshafungwa tangu Ijumaa iliyopita kati ya wiki moja hadi mbili zikiwaacha wanafunzi wa darasa la saba wakikamilisha hatua za mwisho mwisho kabla ya kufanya mtihani wao.

 Akizungumza jana  kwa simu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya High Mount iliyoko Guluka Kwalala Kata ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam, George Mgombozi alisema: “Kwa sasa tunawajenga wanafunzi kisaikolojia baada ya kuwapika vya kutosha.  “Kimsingi, tunachowaambia wanafunzi ni kwamba watambue kuwa wanapofanya mitihani yao waone kama mitihani ya kawaida tu wanayoifanya kila siku,” alisema.
Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mloganzila iliyoko Wilaya  Kisarawe Mkoa wa Pwani, Grace Msele amewataka wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kutumia siku mbili zilizobaki kujiandaa kisaikolojia na  kujiepusha na michezo ya hatari kabla ya kuanza  mitihani yao. Akizungumza kwenye kikao cha wazazi shuleni hapo juzi, Msele alisema kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kuwa karibu na watoto wao katika kipindi hiki ili kuwajengea uwezo.

Mtoto wa Kitanzania

No comments:

Post a Comment