Sunday 15 September 2013

Dawa ya mifugo yatengenezea gongo Dar

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiahidi kuongeza nguvu katika vita dhidi ya wauza dawa za kulevya nchini,
imebainika kuwa kuna mtandao wa wafanyabiashara wa pombe haramu ya gongo unaopika na kuichanganya na dawa za mifugo ili kuiongezea ukali.
Mtandao huo unaomiliki mitambo ya kupika gongo katika eneo la Mto Kizinga uliopo Dambweni, Kata ya Kilungule, wilayani Temeke, unadaiwa kuchanganya pombe hiyo na dawa ya mifugo aina ya Multivitamin ambayo hutumika kurutubisha wanyama.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa dawa hiyo huchanganywa na dawa nyingine ambayo haikufahamika mara moja, kisha kuiweka kwenye gongo ili kuiongezea ukali zaidi.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakipika gongo hiyo katika eneo hilo kwa miaka zaidi ya 10, huku baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa wakitajwa kuwalinda.
Kwa mujibu wa uchunguzi, eneo hilo lina mitambo zaidi ya minne ya kutengeneza gongo na kila mtambo unazalisha pipa moja lenye ujazo wa lita 200.
Mtambo wa gongo
Uchunguzi ulibaini kuwa kila siku wanazalisha zaidi ya lita 800 za gongo ambayo huuzwa kwa rejareja na jumla. Bei ya rejareja kipimo kinaanzia Sh500 hadi Sh5,000, ambapo bei ya jumla ni Sh38,000 kwa ndoo yenye ujazo wa lita 20.
Kwa mtu anayefika kwa mara ya kwanza eneo hilo atakutana na makundi ya watu wakiwa chini ya miti wakijipumzisha wakati wakisubiri pombe hiyo kuwa tayari, huku wakazi wengine wa eneo hilo wakionekana kuendelea na shughuli zao kwenye bustani za mboga za majani zilizolimwa kando kando ya mto.
Mbali ya kuwa wanalindwa na baadhi ya viongozi wa mtaa, wameweka ulinzi wao wenyewe, kwa kuweka vijana zaidi ya 10 ambao hukaa katika eneo hilo kuhakikisha kuwa mtu anayefika katika eneo hilo wanamtambua.
Ukifika katika eneo ilipo mitambo yao, watu wanaofanya kazi ya kupika ni wacheshi, wanaojaribu kumsalimia kila mpita njia bila ya kuwa na hofu yoyote, huku mmojawao ambaye jina lake halikufahamika mara moja akisema kuwa wao ndio waliotengeneza barabara ya kupita magari inayoingia sehemu hiyo.
Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema watu hao ndiyo wasambazaji wakubwa wa gongo jijini Dar es Salaam.
“Biashara hii inalipiwa ‘kodi’ kila mwezi, hawa jamaa huchangishana fedha halafu huwapelekea baadhi ya askari ambao huwalinda wasikamatwe, kuna wakati huchanga hadi laki tatu. Vigumu sana kukamatwa,” alisema.
Gongo inavyotengenezwa

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini pombe hiyo inatengenezwa kwa kutumia malighafi mbalimbali ikiwamo mapapai yaliyooza, vitambaa vichafu vilivyovunda, mihogo na wakati mwingine kinyesi cha binadamu hasa wakati bidhaa nyingine zinapoadimika.
Mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) alisema amekuwa akipika gongo na kuigawa katika madaraja matatu; iliyopikwa kwa mapapai yaliyooza ndiyo inayopendwa zaidi na wateja wake ikilinganishwa na iliyotumia malighafi nyingine.
“Sisi tunatumia mapapai yaliyooza, tunaongeza na sukari pamoja na hamira, ikishaiva tunaitenga kutokana na madaraja yake. Gongo ya eneo hili inasifika sana kwa sababu ya ubora wake, hatuna tatizo la ukosefu wa maji kama walilonalo wenzetu ndiyo maana unaona tunaung’ang’ania huu mto hapa,” alisema na kuongeza :
“Kama mapapai yakiadimika sana, tunaweza kupika kwa kutumia vitambaa vichafu au mihogo.”
Akifafanua alisema wamekuwa wakitembea kwenye madampo kuokota vitambaa pamoja na takataka nyingine, kisha huziloweka kwenye maji kwa muda mrefu hadi zivunde ndipo huwa tayari kwa kupikia gongo.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya pombe hiyo kutengenezwa kwa kutumia takataka zinazookotwa kwenye madampo, pia huongezewa ukali kwa kutumia dawa za kuongezea vitamini mifugo.
Mteja mmoja wa pombe hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Sadick, alisema gongo inayopikwa eneo hilo imekuwa maarufu kwa kuwa kuna dawa ya mifugo ya Multivitamin ambayo huongezwa baada ya pombe hiyo kuiva.
“Mimi ninafahamu kuna dawa ya mifugo inawekwa kwenye hii gongo ili kuiongezea nguvu. Sijui ni dawa aina gani, lakini kuna jamaa huwa namwona anakuja kuuza hiyo dawa. Gongo iliyowekwa hiyo dawa inakuwa na nguvu sana,”alisema Sadick.
Mtaalamu wa Mifugo, Joseph Nong’ona alisema wanywaji wa pombe hiyo wapo katika hatari ya kudhurika kiafya kwa kuwa dawa ya Multivitamin inayotolewa kwa wanyama ina nguvu zaidi ikilinganishwa na ya binadamu, na kwamba mtu haruhusiwi kunywa maziwa au nyama ya mnyama aliyepewa dawa hiyo kwa siku tatu.
“Multivitamin anayopewa mnyama ina ‘concentration’ kubwa ikilinganishwa na ile ya binadamu, lakini pia ikumbukwe kuwa ile ni kemikali sijui inakuwaje inapochanganywa na gongo ambayo yenyewe tu ina madhara makubwa kiafya. Kwa kawaida mnyama akipewa dawa hiyo huwa tunashauri asikamuliwe mazima au nyama yake isitumike kwa siku tatu,” alisema Nong’ona.
Akizungumzia biashara hiyo, Katibu wa Mtaa wa Kilungule, Juma Ahmed aliwatetea wafanyabiashara hao kwa madai kuwa hajawahi kupata taarifa zozote za kufanya uhalifu badala yake wamekuwa walinzi wa amani katika mtaa huo.“Ni watu wazuri sana, sijawahi kusikia wamefanya jambo lolote baya, kwanza wamegeuka kuwa walinzi wa amani hapa mtaani kwetu… wanajua biashara wanayoifanya siyo halali kwa hiyo hawataki matatizo na mtu,” alisema Ahmed.
Kamanda wa Polisi wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema suala la biashara ya gongo linatakiwa kudhibitiwa na jamii inayowazunguka wafanyabishara hao kwa kutumia ulinzi shirikishi.

“Wanataka kuipa Polisi kazi bure tu, jamii ndiyo inayohusika na suala hilo. Serikali ya mtaa kwa njia ya ulinzi shirikishi wanaweza kuamua kwenda kuvunja mitambo ya gongo,” alisema Kiondo.
Akizungumzia tuhuma kuwa baadhi ya Polisi wanawalinda wafanyabiashara wa gongo, Kiondo alisema tuhuma hizo zimekuwepo muda mrefu na kwamba zimeshapitwa na wakati.

No comments:

Post a Comment