Waliovamia mgodi Handeni
waomba muda zaidi
kuondoka
Wachimbaji wadogowadogo wa madini aina ya dhahabu, waliopo katika machimbo maarufu ya Magambazi Magamba wilayani Handeni, wameiomba Serikali kuwapa muda wa miezi sita, kabla ya kuondoka katika eneo hilo.
Wameamua kufanya hivyo kutokana na kutakiwa
kuondoka kwenye machimbo hayo kwa hiari ifikapo Machi 21, mwaka huu na
kuonywa kwamba kama wasipotekeleza agizo hilo wataondoshwa kwa nguvu,
kwa madai kwamba eneo hilo linamilikiwa na mwekezaji.
Ombi hilo walilitoa juzi kwa nyakati tofauti
walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea machimbo
hayo na kujionea mitambo ya wachimbaji hao ikiendelea kusaga mawe ya
madini hayo, huku wengine wakijiandaa kuondoka.
“Sisi tumekaa hapa kwa miaka karibu 10 kwanza hata
sisi tumepachoka kuishi hapa, tunafahamu kwamba hapa tulipo ni kwa mtu
ambaye ana miliki eneo hili.
Lakini kwa vile tuna mitambo yetu na rundo la mawe
kama mnavyoona, hatuwezi kuondoka kwa muda wa siku hizi nne tulizopewa
ambazo zimeisha,” alisema Andrew Rulu.
Katibu wa wachimbaji hao katika machimbo hayo John
Denis, alisema kwamba hawakatai kuondoka hapo, ila wapewe muda kwa
ajili ya kuhamisha virago vyao, ili kwenda kuanza maisha ya kuwekeza
sehemu nyingine.
Akizungumzia wachimbaji hao, mmiliki wa eneo hilo
Rais wa Kampuni ya Canaco nchini, Denis Dillip, alilalamikia baadhi ya
viongozi wa juu serikalini, kwa kushindwa kuwaondoa wachimbaji hao tangu
mwaka 2008, akisema kuwa ana shaka kwamba ndani yake kuna mkono wa
rushwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Muhingo
Rweyemamu, alisema kwamba hataongeza muda mwingine wa wachimbaji hao
kuondoka, akisema kwamba tayari walishapewa barua za kutakiwa kuondoka
tangu mwaka 2009/10, lakini hawakutii.
Rweyemamu alisema wachimbaji wenye Leseni
wamewapangia maeneo mengine ya kuchimba, kwa madai kwamba hawawezi kutoa
leseni juu ya leseni.
No comments:
Post a Comment