Mtwara. Wakati hofu ikiwa imetanda miongoni mwa wananchi, Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji leo anatarajia kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma za uchochezi wa vurugu za kupinga mradi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.
Murji alikamatwa juzi saa kumi na moja jioni, nyumbani kwake eneo la Shangani, Mtwara akituhumiwa kutoa kauli za uchochezi zilizohamasisha vurugu za wananchi Mei, 22, mwaka huu na kusababisha vifo, uharibifu wa mali za raia na Serikali.
MBUNGE WA MTWARA |
“Ni kweli tumemkamata na kwa sasa yupo mahabusu, tunaendelea na mahojiano iwapo tutakamilisha, kesho (leo) tutamfikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,”
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema.
Murji anahusishwa na uchochezi kutokana na uamuzi wake wa kuitisha mkutano wa ndani katika Ukumbi wa Kanisa la Pentekosite, Mtwara Desemba, 31 mwaka jana na kutangaza kuwaunga mkono wananchi katika msimamo wao wa kupinga mradi wa bomba la gesi.
Katika hatua nyingine, watuhumiwa 91 wa vurugu hizo wanatarajia kufikishwa mahakamani kwa mara nyingine leo kusikiliza kesi inayowakabili huku viongozi wengine wa vyama vya siasa vya upinzani nao wakitarajiwa kufikishwa mahakamani Alhamisi ijayo.
Viongozi hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara.
Hofu yatawala
Hofu imetawala miongoni mwa wananchi wa Mjini Mtwara baada ya kusambaa kwa habari kuwa leo shughuli zote za kijamii zitasimamishwa ili kutoa fursa ya wananchi kwenda mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili wenzao. Mwandishi wetu ameshuhudia wakazi wengi wakihamisha familia zao kwenda nje ya Mtwara, wakihofia usalama wao.
“Tunakwenda kutafuta hifadhi sehemu nyingine hadi hali itakapotulia,”
alisema Mwajuma Saleh akiwa Kituo Kikuu cha Mabasi.
Akizungumzia tishio hilo, Kamanda Sinzumwa aliwataka wananchi kuondoa hofu na kutoa wito kwa watoa huduma za jamii kuendelea na shughuli zao.
Katika siku za karibuni kumekuwa na ujumbe mfupi wa simu ambao umekuwa ukisambazwa ukitoa wito kwa wakazi wa Mtwara kukaa nyumbani leo kupinga ujenzi wa bomba hilo.
Polisi wamekuwa wakipita katika mitaa mbalimbali ya Mtwara wakitangaza:...
“Tangazo, tangazo! Tunawatangazia wananchi wote kuwa uvumi na vitisho vinavyoenea kuwa siku ya Jumatatu, Juni 10 mwaka huu, msitishe huduma zote za kijamii ili muende Mahakamani kusikiliza kesi ya watu waliokamatwa kutokana na vurugu zilizotokea Mei 22 mwaka huu; msikubali kabisa ... na mwendelee na shughuli zenu za kila siku,”
alisema mtangazaji akiwa kwenye gari lililokuwa likisindikizwa na magari mawili ya jeshi.
No comments:
Post a Comment