Taifa
Stars wafanyiwa 'umafia'
Morocco,
hali ya wasiwasi yatanda
Kocha wa Stars, Kim Poulsen
Marakech, IMEWEKWA JUNI 8, 2013 SAA 8:00 USIKUTIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars usiku huu imekiona cha moto mbele ya askari wa Uwanja wa Marakech, baada ya kufanyiwa vurugu na kuzimiwa taa ishindwe kufanya mazoezi kwenye Uwanja huo siku moja kabla ya mchezo wao na wenyeji wao Morocco kesho, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia. Sheria za FIFA zinasema timu mgeni, itapewa fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja utakaotumika kwa mechi dhidi ya wenyeji katika muda ambao mechi itachezwa, lakini leo msafara wa Stars ulipofika Uwanja wa Marakech ulizuiwa kuingia ndani na askari wa uwanjani hapo. Juhudi za Kocha mkuu wa Stars, Kim Poulsen kuwaelewesha askari wa Uwanja huo sheria ili wairuhusu timu kuingia uwanjani hazikuzaa matunda na ikabidi viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waingilie kati, nao pia wakachemsha.
Ikawadia zamu ya
viongozi wa Kamati ya Ushindi ya Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premum
Lager, ambao nao walichemsha- ndipo baadhi wa Watanzania waishio hapa na wachache
waliosafiri kutoka Dar es Salaam walipoongeza nguvu.Walikwenda kufungua geti
kwa nguvu, wakawaweka kando askari waliokuwa wanawazuia na kuiingiza timu
uwanjani kufanya mazoezi. Hata hivyo, Stars ilipofika uwanjani ililazimika
kusubiri tena, kwani wenyeji Simba wa Atlasi walikuwa wakiendelea na
mazoezi.Baada ya nusu saa, Morocco walimaliza awamu yao na Stars wakaanza
kupasha misuli moto. Hata hivyo, baada ya dakika 34, taa za Uwanja huo
zilizimwa na uwanjani kuwa giza totoro, lakini viongozi wa TFF wakaenda kuomba,
zikawashwa na timu ikafanya mazoezi kwa dakika 10 zaidi. Naibu Waziri wa Habari
Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makalla aliyekuwapo wakati wa vurumai zote hizo,
alisikitishwa mno na kitendo hicho akisema si cha kiungwana na si cha
kiunamichezo.
Makamu wa Rais wa
TFF, Athumani Nyamlani alisema Morocco walikuja kucheza Dar es Salaam
walipokewa vizuri na wakahudumiwa vizuri hadi wanaondoka, ajabu leo wanaifanyia
‘unyama’ Tanzania.Mkuu wa Msafara wa Stars hapa, Crescentius John Magori
alisema watapeleka malalamiko FIFA, waandaji wa michuano ya kufuzu kwa Kombe la
Dunia na kwa kuwa ushahidi upo, anaamini Morocco watachukuliwa hatua.Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alishauri Stars icheze
chini ya angalizo kwa kuwasilisha barua FIFA mapema ili wakae wanajua kuhusu
hali halisi Morocco.Kwa ujumla kilichotokea leo kimewatia woga Watanzania wengi
waliopo hapa kuelekea mchezo wa kesho, ambao Stars inahitaji ushindi ili
kujiimarisha katika mbio za kuelekea Brazil 2014. Hata ulinzi wa msafara wa
Stars kutoka hotelini hadi uwanjani hakuwa wa kutosha na ilishuhuidiwa mara
kadhaa ukiingiliwa na magari mengine barabarani wakati timu ikienda uwanjani
kwa mazoezi.Wenyeji nchini Morocco wanasema inapowadia mechi, huwa wanaogopa
kwa sababu mara nyingi hutokea vurugu ya damu kumwagika.Kwa ujumla Stars
inaingia katika mchezo wa kesho katika hali ya wasiwasi na woga mkubwa. Stars
itashuka dimbani saa 3:00 usiku kesho kwa saa za hapa sawa na saa 5:00 za
Tanzania kucheza na Morocco.Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa
na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho itakuwa
ugenini ikimenyana na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Stars
ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki moja na
kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya bila
mabao.Kabla ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya
Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya
kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa hotuba
nzuri.
No comments:
Post a Comment