Lissu,Arfi,Mukya,Akunaay watiwa
mbaroni Arusha
Arusha. Wabunge wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu) wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye Uwanja wa Soweto jana.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jana
kwamba pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu wapatao 60 kutokana
na vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi kuwatawanya kwenye uwanja huo
waliokuwa wamekusanyika kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi,
Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea
kwenye uwanja huohuo, Jumamosi iliyopita.
Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
“Tunawasaka wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa kwa kosa la
kuhusika na mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa tumefanikiwa kulinasa
gari la Mbowe,” alisema Chagonja.
Pia kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni
cha Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi walilazimika kutumia nguvu
kuwatawanya waombolezaji hao.
Awali, Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa wamelazimika
kuzuia viwanja hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC kuzuia
shughuli za Chadema kwenye eneo lao.
Kamishna Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari barua aliyosema
imeandikwa na uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea kuutumia Uwanja wa
Soweto.
Mabomu yarindima
Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana asubuhi baada ya
polisi kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa wameanza kufurika
katika eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya maombolezo.
Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya uwanja na kuonekana kama wamewazingira.
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwasili uwanja hapo
yapata saa nane mchana na kukuta zuio hilo na kuanza kuzungumza na
wananchi ingawa FFU walikuwa wakiwataka watu kutawanyika. Mabomu
yalianza kurindima wakati Arfi aliposimama na kuwahimiza wananchi
kuelekea Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu.
“Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba wote tuelekee
Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa sababu uwanja huu
umezuiwa na polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa na milipuko ya
mabomu.Awali, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema alitoa msimamo wa chama hicho kuwa Mwenyekiti wao, Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wa tukio la bomu wala kujisalimisha polisi kwa sababu hawana imani na jeshi hilo.
“Namtaka Chagonja atangulie mahakamani, tutakutana hukohuko. Mbowe na
Lema hawatatoa ushahidi wala kujisalimisha polisi…”
alisema Lissu na kuongeza:
alisema Lissu na kuongeza:
“Kisheria haiwezekani polisi ambao ndiyo watuhumiwa ndiyo wadai kukabidhiwa ushahidi ili wauharibu.”
Mapema Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa
polisi kuhusika na tukio la kurusha bomu kwenye mkutano wa Chadema la
sivyo polisi watatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo.
Hekaheka
Baada ya polisi kuanza kutupa mabomu saa 8.45 mchana, wabunge,
viongozi waandamizi wa Chadema na watu waliokuwa wamekusanyika
walilazimika kutimua mbio.
Watu walioshuhudia tukio lile wanasema viongozi hao akiwamo Mbowe na
mwenzake Lissu walikimbilia kwenye magari yao. Lema alilazimika
kukimbilia kwa wachoma nyama ya nguruwe, (kitimoto) kwenye maeneo ya
Kaloleni.
Kabla ya polisi kurusha bomu mahali alipokuwapo Lema, mbunge huyo alisikika akisema:
“Jaribuni kuvumilia, tunajaribu kuwasiliana Serikali ya Mkoa, ili
watupe kibali cha kuleta miili ya wapendwa wetu hapa, kuweni wastaarabu
kwa sababu mbele yetu kuna wana usalama ambao wanalinda amani, ingawa
kufa ni kufa tu, wenzetu wameshakufa na sisi ipo siku tutakufa, lakini
kila anayetangulia lazima tumzike kwa heshima zote.”
Kauli hiyo iliwachefua polisi ambao walishatangaza amri ya watu
kutawanyika katika viwanja hivyo na kwamba hakutakuwa na suala la kuaga
miili ya watu hao katika eneo hilo. Ghasia hizo zilisababisha kusimama
kwa shughuli za biashara na kijamii kwa muda jijini Arusha huku watu
waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na maeneo yalikorushwa mabomu
wakilazimika kutoka nje kupata hewa safi baada ya nyumba hizo kujaa hewa
ya mabomu.
Polisi waliokuwa wakirusha mabomu waliwakimbiza wananchi hadi maeneo
ya Sakina huku wakiendelea kufyatua mabomu kila walipoona mkusanyiko wa
watu.
Katika eneo la Kaloleni, mkabala na Ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo
baadhi ya wafuasi wa Chadema walichoma matairi barabarani na kusababisha
ifungwe. Pia walichoma matairi katika eneo la Mianzini.Katika eneo la Tanki la Maji, Barabara ya kwenda Moshi, baadhi ya wafuasi wa Chadema walipanga mawe barabarani na kusababisha msongamano wa magari.
Katikati ya jijini Arusha barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na nyingine kufungwa na kusababisha usumbufu mkubwa.
Waandishi nao matatani
Katika vurugu hizo, baadhi ya waandishi wa habari walishambuliwa na
polisi. Hao ni pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti dada la The
Citizen, Zephania Ubwani ambaye kabla ya kuchomoka katika mikono ya
askari, alikuwa akiwaonyesha kitambulisho chake cha kazi.
Hata hivyo, askari hao walimtishia kumtandika na kisha kumwambia aondoke katika eneo hilo kwa kuwa haijalishi yeye ni nani.
Mwingine ni mwandishi wa gazeti la Nipashe, Cnythia Mwilolezi ambaye
alilazimika kuacha viatu na vitendea kazi vyake katika Uwanja wa Soweto
na kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo jirani na eneo la tukio.
Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Moses
Kilyinga alipigwa na polisi baada ya kuonekana akichukua maelezo.
Kilyinga ambaye alishambuliwa na askari hao alisema mara baada ya
askari hao kumkamata, alijitambulisha lakini hawakumwelewa na
wakaendelea kumchapa kabla ya kufanikiwa kuchomoka.
Polisi wavamia hospitali
Wakati baadhi ya majeruhi wakidai kushuhudia polisi wakiwapiga risasi
watu waliokuwa wakimkimbiza mtu aliyerusha bomu katika tukio la
Jumamosi, askari hao juzi walifika katika Hospitali ya Seliani saa mbili
usiku wakitaka kumchukua mmoja wa majeruhi kwa mahojiano kuhusiana na
tukio hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya mgonjwa kutokomea
kusikojulikana baada ya kupata taarifa za kutaka kuhusishwa na tukio
hilo.
Ingawa si polisi wala Chadema waliokuwa tayari kumtaja mgonjwa huyo,
inaelezwa kwamba majeruhi anayesakwa ni Abdallah Alila aliyekaririwa na
vyombo vya habari jana na juzi akidai kumshuhudia aliyerusha boma
akiondoka kwenye moja ya magari ya polisi.Hata hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake linapenda kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika kukusanya ushahidi wake.
No comments:
Post a Comment