Sunday, 15 September 2013

Polisi Simiyu yatoa ripoti ukatili wa Dagashida, fisi wakoleza mauaji



Wiki iliyopita katika ukurasa huu, tuliwaletea mwendelezo wa ripoti maalumu kuhusu mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa mkoani Simiyu kupitia Baraza la Kimila maarufu Dagashida na jinsi wananchi wanavyoogopa kutoa ushirikiano kwa polisi.
Leo tunaendelea na sehemu ya tatu na ya mwisho ya ripoti hiyo, pamoja na mambo mengine ikiainisha takwimu za vifo zilizotolewa na Jeshi la Polisi kutokana na matukio mbalimbali ya mauaji ya Dagashida.
Wanakijiji hawatoi ushirikiano
Kamanda Msangi anakiri kuwepo kwa changamoto ya kukosa ushirikiano kutoka kwa wananchi wakihofia usalama wao.
“Sisi tunawaomba wasiogope kutoa taarifa za ukatili huo, lakini pia tunaomba mashirika na dini waendelee kuelimisha,”anasema Kamanda Msangi.
Anaeleza kusikitishwa kwake na viongozi wa kisiasa kutoshiriki katika harakati za kukemea ukatili wa baraza hilo akifafanua tangu alipoanza kazi mkoani Simiyu hajawahi kuona wala kusikia mbunge yeyote wa mkoa huo akikemea ukatili wa Dagashida.
“Hakuna mbunge au diwani yeyote mwenye nguvu ya kuzuia baraza hilo kwa sababu wanalitumia kisiasa, kwa hivyo niwaombe waache kuchanganya siasa na maisha ya watu. Ni vyema wakashiriki kuelimisha,” anasema.
Polisi na takwimu za mauaji ya Dagashida
Takwimu za Jeshi la Polisi mkoani Simiyu zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji hayo yanahusisha sababu mbalimbali ikiwamo kugombania mirathi, mipaka ya ardhi, imani za kishirikina pamoja na kujichukulia sheria mkononi.
Wiki iliyopita Mkuu wa Polisi Mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi Salum Msangi alisema: “Nilipoingia Simiyu hali ilikuwa mbaya sana. Tulipokea ripoti za matukio kama hayo, hata ya watu watano kuuawa kwa siku, kuona hivyo kwa kushirikiana na mkuu wa mkoa tulizunguka Mkoa wa Simiyu wote kupiga marufuku uwepo wa baraza hilo…,”
Maelezo hayo ya Kamanda Msangi yalimaanisha kuwa katika kila siku saba za wiki watu 35 waliuawa mkoani Simiyu na katika mwezi mmoja wastani wa watu 150 waliuawa katika matukio yaliyohusisha kikundi cha Dagashida.
Hata hivyo, takwimu za jeshi hilo zilizotolewa wiki hii zinabainisha kwamba jumla ya watu 117 ameuawa katika vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Simiyu kati ya Juni 2012 hadi Juni 2013.

Vifo hivyo ni wastani wa vifo vya wanakijiji 10 katika vijiji 12 vilivyo katika mkoa huo, ambao ulitokana na sehemu za Mkoa wa Shinyanga na ule wa Mwanza zilizomegwa na kuanzisha Mkoa wa Simiyu.
Akifafanua kuhusu mauaji hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi Salum Msangi anabainisha kuwa jeshi lake limewatia mbaroni watu 102 na kufikishwa katika vyombo vya sheria wakihusishwa na mauaji hayo.
Mauaji ya kishirikina
Idadi kubwa ya wakazi wa vijiji vya Simiyu wanakiri utekelezaji wa mauaji hufanywa na Baraza la Kimila la Dagashida, huku waathirika wakihusishwa na tuhuma za kishirikina.
Duru zinasema idadi kubwa ya waliouawa ni wanawake wakituhumiwa zaidi kuhusika na matukio ya kishirikina.
Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, katika kipindi cha Juni 2012 hadi Juni 2013, wanakijiji 44 sawa na wastani wa watu watatu, waliuawa kila mwezi kwa tuhuma za ushirikina.Hata hivyo, Kamanda Msangi anasema kuwa rekodi za matukio ya kishirikina zinaonekana kupungua kwa kasi ukilinganisha na kipindi cha mwezi Juni mwaka jana.
“Juni mwaka jana wanakijiji 9 waliuawa ila kadri tunavyozidi kudhibiti, idadi inapungua na kwa mwezi Juni mwaka huu hakuna aliyeuawa kwa tuhuma za tukio kama hilo,” anasema.
Aliongeza kuwa mbali ya takwimu kuonyesha matumaini, hali bado siyo nzuri kwa baadhi ya vijiji hasa Wilaya ya Itilima.
“Huko ndiyo bado wanavichwa vigumu hawataki kubadilika, lakini tutahakikisha wanakoma,” anasema Kamanda Msangi.
Akichangia taarifa za mauaji hayo, Emmanuel Magunzagula mmoja wa wanakijiji wa Nyamiswi, Kata ya Gambushi, anasema kuwa kupitia Dagashida hilo, wamekuwa wakisadiki kuwa mwanamke pekee ndiyo mshirikina.
“Ukisikia mwanakijiji ameuawa kwa tuhuma za ushirikina basi atakuwa ni mwanamke, sijawahi kuona mwanamume ameuawa kwa tuhuma hizo hapa kijijini,” anasema Magunzagula na kuongeza: “Dhana hiyo inatokana na mfumo dume uliojengeka katika jamii.”
Anaongeza kuwa utekelezaji wa hukumu hizo unapofanyika, unaweza kusababisha familia yote kuuawa kwa mapanga.

“Mwanamke anayetuhumiwa anaweza kuuawa yeye na watoto wake wote, hawaangalii kama mtoto hana kosa, wao ni mapanga tu,” anasema Magunzagula.
Fisi wakoleza mauaji
Moja ya sababu kubwa inayotajwa kuchangia mauaji hayo ni wanakijiji wengi kupoteza maisha kwa kuliwa na mnyama fisi.
Chanzo chetu cha habari mkoani humo kinaeleza kuwa hadi sasa kuna matukio 40 ya wanakijiji kuliwa na fisi katika maeneo ya vijiji mbalimbali mkoani humo, huku jamii ikiamini kwamba mtu kuliwa na fisi hutokana na vitendo vya kishirikina.
“Kesi zipo, lakini hakuna ushahidi wa nani aliyehusika kwa sababu fisi wamezagaa sana mitaani, asubuhi saa moja unaweza kupishana na fisi, hivyo inaweza kuwa siyo ajabu watu kulia na fisi kutokana na mazingira hayo,” anasema Magunzagula.
Ugomvi wa mali na mipaka ya ardhi
Mauaji yatokanayo na ugomvi wa mipaka ya ardhi pia ni moja ya adha inayodaiwa kuwaathiri wanyonge tu katika mauaji hayo ya Dagashida.
Baraza la Dagashida limekuwa likituhumiwa kutumika kama silaha ya kulipiza kisasi miongoni mwa wanakijiji wanaogombania mipaka ya ardhi.
Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa katika mwaka mmoja uliopita (Juni 2012/13), wanakijiji 30 waliuawa wakati wakigombea mali, huku wengine 16 wakiuawa katika matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi.
“Kwa hivyo ni wanakijiji 46 waliouawa ambao ni sawa na wastani wa wanakijiji wanne kila mwezi, hali hiyo bado ni mbaya. Lakini tunaendelea taratibu kuondoa changamoto hiyo kwa njia za kuelimisha na kuwachukulia hatua za kisheria,” anasema Kamanda Msangi.
Dini zinahitajika
Dini imetajwa kuwa moja kati ya njia kuu inayoweza kutumika kupunguza au kuondoa mila potofu zinazoshinikizwa na Dagashida.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Biashara iliyopo wilayani Bariadi, Emmanuel Bujiku anasema kuwa imani za dini zikienezwa ipasavyo Simiyu itasaidia jamii kumjua Mungu na kustaarabika.
“Watu wakiwa na imani za dini, iwe ya Kikristo au Kiislamu watakuwa wakiishi kwa hofu ya Mungu, hata mauaji haya yatapungua na kumalizika kabisa,” anasema Bujiku.
Kwa mujibu wa mazingira na uzoefu alionao mkoani humo, Bujiku anasema kuwa kwa sasa kati ya wanafunzi 50, watatu ndiyo wanajua dini. Akikiri hali hiyo, Kamanda Msangi anabainisha kuwa moja kati ya changamoto iliyopo maeneo mengi ya Mkoa wa Simiyu ni watu kutokuwa na imani za kidini.
“Hilo nalo ni tatizo, siyo wanakijiji tu, hata mwenyekiti au mtendaji wa kijiji hajui dini yoyote,” anasema.
Wabunge wa Simiyu
Kwa nyakati tofauti wananchi wa mkoa wa Simiyu wamewataka wabunge watano wa majimbo ya mkoa huo kushiriki katika harakati za kupambana na ukatili unayofanywa na Dagashida, wakiwataka pia viongozi wanaolitumia kisiasa baraza hilo kuacha mara moja.

No comments:

Post a Comment