Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiahidi kuongeza nguvu katika
vita dhidi ya wauza dawa za kulevya nchini,
imebainika kuwa kuna mtandao wa wafanyabiashara wa pombe haramu ya gongo unaopika na kuichanganya na dawa za mifugo ili kuiongezea ukali.
imebainika kuwa kuna mtandao wa wafanyabiashara wa pombe haramu ya gongo unaopika na kuichanganya na dawa za mifugo ili kuiongezea ukali.
Mtandao huo unaomiliki mitambo ya kupika gongo
katika eneo la Mto Kizinga uliopo Dambweni, Kata ya Kilungule, wilayani
Temeke, unadaiwa kuchanganya pombe hiyo na dawa ya mifugo aina ya
Multivitamin ambayo hutumika kurutubisha wanyama.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
umebaini kuwa dawa hiyo huchanganywa na dawa nyingine ambayo
haikufahamika mara moja, kisha kuiweka kwenye gongo ili kuiongezea ukali
zaidi.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakipika gongo hiyo
katika eneo hilo kwa miaka zaidi ya 10, huku baadhi ya viongozi wa
serikali ya mtaa wakitajwa kuwalinda.
Kwa mujibu wa uchunguzi, eneo hilo lina mitambo
zaidi ya minne ya kutengeneza gongo na kila mtambo unazalisha pipa moja
lenye ujazo wa lita 200.
Mtambo wa gongo |
Kwa mtu anayefika kwa mara ya kwanza eneo hilo
atakutana na makundi ya watu wakiwa chini ya miti wakijipumzisha wakati
wakisubiri pombe hiyo kuwa tayari, huku wakazi wengine wa eneo hilo
wakionekana kuendelea na shughuli zao kwenye bustani za mboga za majani
zilizolimwa kando kando ya mto.
Mbali ya kuwa wanalindwa na baadhi ya viongozi wa
mtaa, wameweka ulinzi wao wenyewe, kwa kuweka vijana zaidi ya 10 ambao
hukaa katika eneo hilo kuhakikisha kuwa mtu anayefika katika eneo hilo
wanamtambua.
Ukifika katika eneo ilipo mitambo yao, watu
wanaofanya kazi ya kupika ni wacheshi, wanaojaribu kumsalimia kila mpita
njia bila ya kuwa na hofu yoyote, huku mmojawao ambaye jina lake
halikufahamika mara moja akisema kuwa wao ndio waliotengeneza barabara
ya kupita magari inayoingia sehemu hiyo.
Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake
liandikwe gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema watu hao ndiyo
wasambazaji wakubwa wa gongo jijini Dar es Salaam.
“Biashara hii inalipiwa ‘kodi’ kila mwezi, hawa
jamaa huchangishana fedha halafu huwapelekea baadhi ya askari ambao
huwalinda wasikamatwe, kuna wakati huchanga hadi laki tatu. Vigumu sana
kukamatwa,” alisema.
Gongo inavyotengenezwa
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini pombe hiyo
inatengenezwa kwa kutumia malighafi mbalimbali ikiwamo mapapai
yaliyooza, vitambaa vichafu vilivyovunda, mihogo na wakati mwingine
kinyesi cha binadamu hasa wakati bidhaa nyingine zinapoadimika.
Mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) alisema
amekuwa akipika gongo na kuigawa katika madaraja matatu; iliyopikwa kwa
mapapai yaliyooza ndiyo inayopendwa zaidi na wateja wake ikilinganishwa
na iliyotumia malighafi nyingine.
“Sisi tunatumia mapapai yaliyooza, tunaongeza na
sukari pamoja na hamira, ikishaiva tunaitenga kutokana na madaraja yake.
Gongo ya eneo hili inasifika sana kwa sababu ya ubora wake, hatuna
tatizo la ukosefu wa maji kama walilonalo wenzetu ndiyo maana unaona
tunaung’ang’ania huu mto hapa,” alisema na kuongeza :
“Kama mapapai yakiadimika sana, tunaweza kupika kwa kutumia vitambaa vichafu au mihogo.”
Akifafanua alisema wamekuwa wakitembea kwenye
madampo kuokota vitambaa pamoja na takataka nyingine, kisha huziloweka
kwenye maji kwa muda mrefu hadi zivunde ndipo huwa tayari kwa kupikia
gongo.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya
pombe hiyo kutengenezwa kwa kutumia takataka zinazookotwa kwenye
madampo, pia huongezewa ukali kwa kutumia dawa za kuongezea vitamini
mifugo.
Mteja mmoja wa pombe hiyo ambaye alijitambulisha
kwa jina moja la Sadick, alisema gongo inayopikwa eneo hilo imekuwa
maarufu kwa kuwa kuna dawa ya mifugo ya Multivitamin ambayo huongezwa
baada ya pombe hiyo kuiva.
“Mimi ninafahamu kuna dawa ya mifugo inawekwa
kwenye hii gongo ili kuiongezea nguvu. Sijui ni dawa aina gani, lakini
kuna jamaa huwa namwona anakuja kuuza hiyo dawa. Gongo iliyowekwa hiyo
dawa inakuwa na nguvu sana,”alisema Sadick.
Mtaalamu wa Mifugo, Joseph Nong’ona alisema
wanywaji wa pombe hiyo wapo katika hatari ya kudhurika kiafya kwa kuwa
dawa ya Multivitamin inayotolewa kwa wanyama ina nguvu zaidi
ikilinganishwa na ya binadamu, na kwamba mtu haruhusiwi kunywa maziwa au
nyama ya mnyama aliyepewa dawa hiyo kwa siku tatu.
“Multivitamin anayopewa mnyama ina ‘concentration’
kubwa ikilinganishwa na ile ya binadamu, lakini pia ikumbukwe kuwa ile
ni kemikali sijui inakuwaje inapochanganywa na gongo ambayo yenyewe tu
ina madhara makubwa kiafya. Kwa kawaida mnyama akipewa dawa hiyo huwa
tunashauri asikamuliwe mazima au nyama yake isitumike kwa siku tatu,”
alisema Nong’ona.
Akizungumzia biashara hiyo, Katibu wa Mtaa wa
Kilungule, Juma Ahmed aliwatetea wafanyabiashara hao kwa madai kuwa
hajawahi kupata taarifa zozote za kufanya uhalifu badala yake wamekuwa
walinzi wa amani katika mtaa huo.“Ni watu wazuri sana, sijawahi kusikia
wamefanya jambo lolote baya, kwanza wamegeuka kuwa walinzi wa amani hapa
mtaani kwetu… wanajua biashara wanayoifanya siyo halali kwa hiyo
hawataki matatizo na mtu,” alisema Ahmed.
Kamanda wa Polisi wa Temeke, Engelbert Kiondo
alisema suala la biashara ya gongo linatakiwa kudhibitiwa na jamii
inayowazunguka wafanyabishara hao kwa kutumia ulinzi shirikishi.
“Wanataka kuipa Polisi kazi bure tu, jamii ndiyo inayohusika na
suala hilo. Serikali ya mtaa kwa njia ya ulinzi shirikishi wanaweza
kuamua kwenda kuvunja mitambo ya gongo,” alisema Kiondo.
No comments:
Post a Comment