Tanzania: Hatutavumilia
wahamiaji haramu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchini Tanzania imetoa tamko kwa
wahamiaji haramu kurejea makwao mara moja kwa hiyari, kwani zoezi la
kuwasaka na kuwarejesha litaanza wakati wowote kuanzia sasa. Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Dk. Emmanuel Nchimbi amesema tayari amekabidhiwa na Rais Jakaya Kikwete
jukumu la kuwahamisha wahamiaji haramu waliopo katika mikoa ya Kagera,
Kigoma na Geita. Kauli hiyo ya Dk. Nchimbi imekuja baada ya wiki mbili
alizotoa Rais Jakaya Kikwete kwa wahamiaji hao kumalizika. Rais Kikwete
alipokuwa mkoani Kagera Julai 29 mwaka huu, alitoa tamko kwa wahamiaji
wote haramu waliopo katika mkoa huo na maeneo jirani kufunga virago na
kurejea makwao. Wahamiaji hao haramu waliorejea makwao ni kutoka nchi za
Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Dk.
Nchimbi amesema, wakati wa wahamiaji haramu kurejea makwao ni sasa,
kwani Tanzania haitavumilia tena wahamiaji haramu. Ameongeza kuwa,
wahamiaji haramu wanaotaka kuishi Tanzania warejee makwao, kisha wafuate
taratibu za kuingia na kuishi Tanzania.