WANAOTAFUTA KAZI NI WENGI, AJIRA NI CHACHE
WANAOTAFUTA KAZI NI WENGI,
Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA), imesema inakabiliwa na
changamoto mbalimbali, ikiwamo kutokuwa na fursa za kazi za kutosha
ukilinganisha na idadi ya wahitimu/watafuta kazi waliopo katika soko la
ajira.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam,
Msemaji wa TAESA, Peter Ugater, alisema kwa sasa wahitimu na watafuta
ajira wamekuwa ni wengi kulinganisha na nafasi za kazi zilizopo.
Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni kutokuwa na rasilimali za kutosha
kuwezesha kufikia malengo ya wakala, watafuta kazi wengi kuwa na
matarajio makubwa kuliko hali halisi ya soko la ajira, pia baadhi ya
waajiri na watafuta kazi kutotumia huduma za wakala nchini.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Peter Ugater alisema TAESA ina
mikakati mbalimbali kama vile kukusanya, kuchambua na kusambaza taarifa
za soko la ajira na kuendeleza rasilimali watu ili kuongeza tija na
ufanisi.
Nyingine ni kuendelea kuwaunganisha watafutakazi na
waajiri ndani na nje ya nchi na kufanya utafiti katika Nyanja za
upatikanaji wa fursa za ajira pamoja na kuendelea kuainisha wakala
binafsi kwa lengo la kutoa huduma hiyo nchi nzima.
Pia, Ugater
alisema mpaka sasa TAESA imeshawahudumia jumla ya wateja 13,188 kati
yao ikiwa watafutakazi 1,229, waajiri 830 na wakala binafsi 60 na
kuendesha vipindi kwa watafutakazi 426 kwa lengo la kuwajengea uwezo wa
kuhimili ushindani na changamoto zilizopo katika soko la ajira.
No comments:
Post a Comment