MAJANGA : Mhadhiri UDSM auawa kinyama Dar,Wazungu wamwagiwa tindikali Z'bar,JK asema tukio limeitia aibu nchi
Dar/Zanzibar.
Mauaji, mashambulizi ya kudhuru mwili na uporaji vimeendelea kuchafua taswira ya Tanzania baada ya juzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuuawa kwa kupigwa risasi na watu ambao hawajafahamika, raia wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali na mfanyabiashara kuporwa zaidi ya Sh40 milioni.
Jana, Rais Jakaya Kikwete alikwenda Hospitali ya
Aga Khan kuwajulia hali raia hao wawili wa Uingereza waliomwagiwa
tindikali huko Zanzibar, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) akisema
tukio hilo limetia aibu kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi
kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
Mauaji
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Camillius Wambura alisema jana kuwa mauaji ya Mhadhiri huyo Msaidizi
katika Idara ya Uhandisi na Teknolojia, Patrick Rweyongeza (32)
yalitokea juzi saa saba mchana maeneo ya Magomeni Tanesco, Dar es
Salaam, wakati marehemu alipokuwa ndani ya gari lake akielekea katikati
ya jiji.
“Alipofika maeneo hayo alivamiwa na watu waliokuwa
kwenye pikipiki aina ya Boxer ambao walimpiga risasi ya kifua upande wa
kulia kisha kutokomea.”
“Baada ya kupigwa risasi alipelekwa Muhimbili
lakini kabla ya kuanza kupatiwa matibabu alifariki dunia,” alisema
Kamanda Wambura.
Alisema hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kuhusiana
na tukio hilo. “...Tunaendelea na upelelezi kufahamu tukio hilo
lililofanywa na watu hao kama ni la ujambazi au kisasi.”
Akizungumza nyumbani kwa mjomba wa marehemu
Mbweni, Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Uhandisi, Dk John Mahunza
alisema Rweyongeza alikutwa na mkasa huo baada ya kutoka benki kuchukua
fedha kwa ajili ya shughuli za ofisi.
“Baada ya kuchukua fedha hizo Ubungo, alipanda
gari kuelekea Magomeni na kufika maeneo ya Tanesco, walimzingira na
kumlazimisha kufungua mlango, lakini aligoma na wakampiga risasi,”
alisema.
“Baada ya kumpiga risasi mkononi, walimpora
bahasha iliyokuwa na fedha... nadhani wale walikuwa wanamfuatilia tangu
alipokuwa benki hadi anatoka.
Dk Muhunza alisema marehemu alipata shahada yake ya kwanza mwaka
2004 chuoni hapo na baadaye shahada ya uzamili katika chuo kimoja cha
London, Uingereza. Alifundisha chuoni hapo masomo ya Numerical Method na
Building Design kwa miaka mitatu.
“Marehemu alikuwa na mpango wa kwenda kuchukua shahada ya uzamivu katika chuo kimoja London na alikuwa hajaoa.”
Msemaji wa familia, Damas Kayanda alisema marehemu
anatarajiwa kuagwa leo kwa shughuli za ibada kufanyika katika Kanisa la
Mtakatifu Raphael na kesho utasafirishwa kwenda Tabora kwa maziko.
Tindikali
Wasichana hao wawili walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe wakiwa katika matembezi ya kawaida juzi usiku.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Mkadamu Khamis Mkadamu alisema tukio hilo lilifanywa na vijana wawili
waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa.
Mkadamu alisema Wazungu hao walikuwa walimu wa kujitolea katika Shule St Monica, Tomondo, Zanzibar.
Alisema waathirika hao wamedhurika kiasi kikubwa
katika maeneo ya kifua na mikononi na baada ya tukio hilo, walipelekwa
Hospitali Kuu ya Zanzibar na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Aga Khan,
Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Mganga Mkuu wa Aga Khan, Dk Jaffery Dharsee
alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na hali za wasichana hao akisema
hajapata ruhusa kutoka kwa ndugu wa familia.
Maofisa mbalimbali wa Ubalozi wa Uingereza nchini walifika hospitalini hapo kuwajulia hali wagonjwa hao.
Uporaji
Majambazi wanne walimvamia mfanyabiashara wa vifaa vya magari na kumpora zaidi ya Sh40 milioni alizokuwa akipeleka benki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marieta
Minangi alisema tukio hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi kwenye
makutano ya Mitaa wa Livingstone na Kiungani, Dar es Salaam wakati
mfanyabiashara huyo aliyefahamika kwa jina moja la Bupedra akiwa na
dereva wake kwenye aina ya Toyota Hiace.
Alisema walipofika katika eneo hilo walivamiwa na
watu wanne waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Boxer na walisimamisha gari
hilo kisha kupiga risasi moja hewani na kuvunja kioo cha dirisha cha
mlango wa mbele kwa nondo na kumtaka Bupedra awape fedha hizo
zilizokuwamo kwenye begi haraka.
“ Watu hawa walikuwa wanajua kila kitu kilichomo
kwa sababu waliposimamisha gari walitaka wapatiwe fedha haraka na
walipatiwa na kutokomea, “ alisema Kamanda Marieta.
Alisema polisi wanamshikilia dereva wa gari hilo kwa upelelezi wa tukio hilo ambalo hakuna mtu aliyejeruhiwa.
No comments:
Post a Comment