Waislamu watakiwa kuenzi maadili ya dini wakati wote
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametoa
zawadi za sikukuu ya Idd El Fitr zenye thamani ya Sh8.5 milioni kwa makundi maalumu, wakiwamo watoto wenye ulemavu, wazee, yatima pamoja na watoto walio katika mkinzano na sheria ili kuwaandalia mazingira mazuri ya kushiriki na kusherehekea sikukuu hiyo.
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Rabikira Mushi
jana kwa niaba ya rais alikabidhi zawadi hizo kwa vituo vya Dar es
Salaam, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Mahabusu ya Watoto Kisutu
na kuhudhuriwa na wawakilishi wa vituo husika.
Alisema, Rais ametoa zawadi ya mchele, mafuta ya
kupikia pamoja na mbuzi kwa baadhi ya vituo vya Pwani, Kagera, Mbeya,
Morogoro, Tanga, Zanzibar na Dar es Salaam.
Kaimu kamishna huyo alivitaja vituo vya jijini Dar
es Salaam vilivyopatiwa zawadi hizo kuwa ni pamoja na Kurasini,
Msongola, Chamanzi na kituo cha ushauri cha vijana cha Temeke.
Vingine ni pamoja na Mahabusu ya Watoto Kisutu,
Mburahati, Msimbazi,Tupendane na Wazee Nunge Kigamboni Chuo cha Ufundi
Stadi kwa wenye Ulemavu Yombo.
Mushi alibainisha kuwa mgawanyo wa zawadi hizo uliangalia idadi ya watoto katika kituo.
Akitoa shukrani baada ya kupokea zawadi, Ofisa
Mfawidhi Jela ya Watoto Upanga, Alex Bwire alisema anamshukuru Rais kwa
kuwapa faraja watoto lakini pia aliiomba jamii nzima ihusike katika
kutoa michango kwa makundi maalumu badala ya kuachiwa Rais pekee.
Pia alizitaja changamoto wanazokumbana nazo katika
mahabusu za watoto kuwa ni pamoja na kupokea idadi kubwa ya watoto
isiyoendana na vyumba vya malazi, lakini pia bajeti ni finyu suala
linalosababisha watoto kukosa baadhi ya mahitaji.
No comments:
Post a Comment