JAPAN YAICHAGUA TANZANIA KUWA
KITOVU CHA BIASHARA AFRIKA
- Kuboresha reli ya kati, bandari ya Dar na kujenga viwanda
Japan imeichagua Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji barani
Afrika, ili kuiwezesha kuwa na uchumi imara na wenye uwezo kuondoa
umaskini na kuongeza fursa za ajira.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana, ilisema katika
kufikia azma hiyo, Japan itasaidia kuboresha reli ya kati, kuipanua
bandari ya Dar es Salaam iwe ya kisasa na kujenga viwanda vikiwamo vya
kutengeneza pikipiki za Honda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,
Tanzania itapata fursa ya kuwa mshirika wa kwanza wa Japan, ikiwa ni
matokeo ya mazungumzo baina ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa
Japan, Shinzo Abe yaliyofanyika Tokyo Juni, mwaka huu.
Uamuzi
huo wa Japan, ulitangazwa rasmi jana Ikulu jijini Dar es Salaam na
Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo, Toshimistu Motegi,
alipozungumza na Rais Kikwete. Motegi, alisema Japan itawatumia
wataalamu wake kuiboresha reli ya kati kwa kujenga njia ya kimataifa
itakayokuwa mbadala wa reli nyembamba iliyopo sasa.
Mazungumzo
hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji
na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda
na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Motegi
ameambatana na wafanyabiashara wa Japan watakaokutana na wale wa ndani,
ikiwa ni moja ya mkakati wa kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika
Afrika kwenye uwekezaji na uchumi ulioimarika.
Waziri huyo pia
alisema Japan imekusudia kuhakikisha bidhaa ambazo zinanunuliwa kutoka
Japan, zinazalishwa hapa nchini kwenye viwanda vitakavyojengwa na
kampuni za nchini humo.
Alisema, kampuni mbili za Honda na Panasonic zitajenga viwanda vya kutengeneza pikipiki za Honda na kuzalisha vifaa vya umeme.
Pia, alisema kadhalika kampuni za Japan zitawekeza kwenye kilimo hasa cha pamba na kuanzisha viwanda vya nguo.
Akiwa Tokyo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Mkuu, Abe kuwekeza zaidi
barani Afrika akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa makubwa duniani
ambayo yamefanikiwa kupata soko Afrika hasa eneo la magari.
No comments:
Post a Comment